26.6 C
New York

Kwa makocha hawa, mbona kazi ipo Kombe la Dunia 2026!

Published:

LONDON, Uingereza

UPEKEE wa fainali za Kombe la Dunia za mwaka huu ni namna zitakavyohusisha makocha wa daraja la juu, pengine kuliko ilivyowahi kutokea katika historia ya mashindano hayo.

Hivyo, fainali za safari hii zitakazoanza Juni 11, 2026 zinatarajiwa kuna na ushindani mkali wa mbinu za uwanjani, hivyo kuziongezea ugumu mbio za kuliwania taji.

CARLO ANCELOTTI

Kocha wa zamani wa Real Madrid, AC Milan, Paris Saint-Germain na Chelsea boss, ambaye ametwaa mara tano taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Muitalia huyo pia ni bingwa wa Ligi Kuu katika nchi zote alizowahi kufanya kazi, yaani Italia (Serie A), England, Ufaransa (Ligue 1), Hispania (La Liga) na Ujerumani (Bundesliga).

Kwa sasa, Ancelotti anaiongoza timu ya Taifa ya Brazil, akiwa kocha wa kwanza wa kigeni kukinoa kikosi hicho.

THOMAS TUCHEL

Ni kocha mwingine mwenye historia ya kutwaa ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya akiwa na Chelsea, pia akiwa na uzoefu wa kuzinoa PSG, Bayern Munich na Borussia Dortmund.

Kwa sasa, kocha huyo raia wa Ujerumani analiongoza benchi la ufundi la timu ya Taifa ya England ‘Three Lions’, ambayo inasaka ubingwa wake wa kwanza wa Kombe la Dunia tangu ilipotwaa mwaka 1966.

Tuchel aliiwezesha timu hiyo kufuzu fainali za mwaka huu ikiwa imeshinda mechi zote nane, pia safu ya ulinzi ikifanikiwa kutokurusu bao.

MAURICIO POCHETTINO

Aliwahi kuwika Ligi Kuu ya England akiwa na Tottenham, kabla ya kuondoka klabuni hapo na kuongeza CV yake kwa kufanya kazi PSG na Chelsea.

Pochettino atakiongoza kikosi cha timu ya Taifa ya Marekani akiwa kwenye nchi, ikiwa ni mara yake kwanza kufanya kazi na timu ya taifa.

Marekani chini ya Muargentina huyo haijawa na matokeo ya kuridhisha, ingawa uzoefu wake unaipa matumaini makubwa kuelekea fainali hizo.

DIDIER DESCHAMPS

Kocha huyo anarejea akiwa na rekodi ya kuipa timu ya Taifa ya Ufaransa ubingwa wa Kombe la Dunia mwaka 2018, kabla ya kuifikisha fainali msimu uliofuata (2022).

Deschamps, kiungo wa ulinzi wa zamani wa timu hiyo, amekuwa kwenye benchi la ufundi kwa miaka 14, hivyo ana uzoefu wa kutosha kuelekea fainali za mwaka huu.

Hizi ni fainali zake za mwisho, kisha atastaafu. Ni wazi atataka kuondoka akiwa na historia nzuri zaidi katika utumishi wake kwenye timu hiyo.

LIONEL SCALONI

Ndiye kocha aliyeiongoza Argentina kutwaa ubingwa wa Kombe la Dunia mwaka 2022, walipoifunga Ufaransa kwa mikwaju ya penalti katika mchezo wa fainali.

Mbali ya Kombe la Dunia, pia kocha mzawa huyo ameiongoza timu hiyo maarufu kwa jina la ‘La Albiceleste’ kutwaa mataji mawili ya Copa America.

Je, Scaloni atalibeba kwa mara ya pili mfululizo Kombe la Dunia? Je, uwepo wa Lionel Messi, ambaye hizi ni fainali zake za mwisho, utamsaidia kocha huyo kuibuka kidedea?

Related articles

Recent articles