Na Ramadhan Hassan, Gazetini-Dodoma
WAZIRI wa Fedha, Khamis Mussa Omar, amesema Serikali itaendelea kutegemea mapato ya ndani kama chanzo kikuu cha kugharamia matumizi ya kawaida na utekelezaji wa miradi ya maendeleo, huku ikiweka mkazo katika kuimarisha ukusanyaji wa mapato hayo ili kuharakisha maendeleo ya taifa.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Juni 10, 2026 jijini Dodoma katika mkutano wa kutoa dondoo za Bajeti Kuu ya Serikali kabla ya kuwasilishwa rasmi bungeni kesho Juni 11, 2026, Waziri huyo amesema zaidi ya asilimia 70 ya bajeti ya mwaka wa fedha 2026/2027 itatekelezwa kupitia mapato ya ndani.
Amesema Serikali itaendelea kuelekeza rasilimali zake katika utekelezaji wa miradi ya kimkakati yenye mchango mkubwa katika kukuza uchumi, kuongeza ajira na kuboresha maisha ya wananchi.
Miongoni mwa miradi hiyo ni ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR), upanuzi na uboreshaji wa mtandao wa barabara nchini, miradi ya maji safi na salama, sekta ya nishati pamoja na uwekezaji mkubwa katika maendeleo ya rasilimali watu kupitia elimu, afya na mafunzo ya ujuzi.
Balozi Omar amesema bajeti ya mwaka 2026/2027 ina umuhimu wa kipekee kwa kuwa ndiyo bajeti ya kwanza kutekeleza kwa vitendo malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, Mpango wa Nne wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano wa mwaka 2026/27 hadi 2030/31 pamoja na Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2025.
Aidha, amesema Serikali imeendelea kuzingatia ushirikishwaji wa wadau mbalimbali katika mchakato wa maandalizi ya bajeti ili kuhakikisha sera za kodi, ada na tozo zinazopendekezwa zinazingatia mahitaji ya wananchi, wawekezaji na sekta ya biashara.
Kwa mujibu wa Waziri huyo, hadi kufungwa kwa dirisha la kupokea maoni ya wadau kuhusu maboresho ya kodi, Serikali imepokea jumla ya mapendekezo 727 kutoka kwa wafanyabiashara, taasisi za umma na binafsi, asasi za kiraia, taasisi za elimu ya juu pamoja na wananchi mmoja mmoja.
Amesema mapendekezo hayo yalifanyiwa uchambuzi wa kina na Kamati ya Wataalam wa Maboresho ya Kodi, ambapo mapendekezo 125 yalikubaliwa kama yalivyowasilishwa huku mapendekezo 121 yakifanyiwa maboresho kabla ya kupitishwa.
Aidha, amesema mapendekezo 295 hayakukubaliwa kutokana na kutokidhi vigezo vya kitaalamu na kutokulingana na maslahi mapana ya taifa. Vilevile, mapendekezo 107 yalipelekwa katika wizara na taasisi husika kwa ajili ya uchambuzi zaidi na utoaji wa ufafanuzi wa kitaalamu.
Balozi Omar ameongeza kuwa mapendekezo mengine 47 yanaendelea kufanyiwa tathmini kutokana na upungufu wa takwimu na taarifa muhimu zinazohitajika kabla ya kufanya maamuzi ya mwisho.


