Na mwandishi wetu, Gazetini
KUFIKIA hatua hii ya msimu wa 2025-26 wa Ligi Kuu Bara, matajiri wa Chamazi, Azam FC, wameruhusu nyavu zao kutikiswa mara tisa pekee katika mechi 25 walizoshuka dimbani.
Kwa hesabu hizo, Azam ya safari hii ni tofauti na ya msimu uliopita, ambapo ilimaliza mechi 30 ikiwa imeruhusu nyavu zake kutikiswa mara 19.
Hata hivyo, bado vijana hao wa kocha Florent Ibenge wana mechi tano za kuhakikisha wanakaza na kutokuruhusu mabao 10 yatakayovunja rekodi yao hiyo ya msimu wa 2024-25.
Wakati huo huo, safari hii safu ya ushambuliaji ya Azam pia inadaiwa mabao 18 ili kufikia idadi iliyofunga msimu uliopita, ambapo ilimaliza ikiwa imezifumania nyavu mara 56.
Kwa upande mwingine, baada ya ushindi mara 14 msimu huu, Azam ina kibarua cha kushinda michezo yote mitano iliyobaki ili kufikia idadi ya mechi 19 walizoshinda msimu uliopita.
Pia, baada ya kufungwa mara moja katika mechi 25 msimu huu, Azam haipaswi kupoteza tena ili kuilinda rekodi yake ya msimu uliopita ilipomaliza mechi 30 ikiwa imechezea vichapo vitano.


