KINSHASA, DRC
MLIPUKO wa ugonjwa wa Ebola umeendelea kuwa gumzo si tu DRC ulikoanzia, bali pia nchi jirani za Afrika, ikiwamo Uganda, na sasa unatishia fainali za Kombe la Dunia za mwaka huu.
Michuano hiyo itaanza Juni 11, 2026, safari hii ikifunga katika mataifa matatu ya Marekani, Mexico na Canada.
Kufikia Juni 4, 2026, taarifa za Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa (WHO) lilieleza kuwa visa vya Ebola nchini DRC vimefikia 381, huku vifo vikiwa ni 62. Idadi ya visa kwa majirani zao, Uganda, ni 16, kwa mujibu wa WHO.
Ni kasi kubwa ya maambukizi ya virusi hivyo tangu kisa cha kwanza kiliporipotiwa nchini DRC Aprili 24, 2026.
HOFU KOMBE LA DUNIA
Wataalamu wa afya, licha ya kuona uwezekano ni mdogo kwa maambukizi kutawala Kombe la Dunia, wanaonya kuwa tahadhari zinapaswa kuchukuliwa.
Hivi karibuni, timu ya soka ya Taifa ya DCR ilishindwa kucheza mechi zake mbili za kujiandaa na fainali hizo kutokana na hofu ya maambukizi ya virusi hivyo vya Ebola.
Ikiwa Hispania kwa kambi ya maandalizi, mamlaka za nchi hiyo zilizuia mechi yao dhidi ya Chile iliyotarajiwa kuchezwa Juni 9, 2026.
Awali, Serikali ya Marekani iliweka wazi kuwa haitoiruhusu DRC kuingia nchini humo bila kukaa karantini kwa walau wiki mbili.
DRC itakuwa mjini Texas wakati wa michuano ya Kombe la Dunia kwa mchezo wa ufunguzi dhidi ya Ureno (Juni 17), kabla ya kuelekea Mexico kwa ajili ya kuivaa Colombia (Juni 24), kisha kurudi Marekani kuikabili Uzbekistan (Juni 28).
Wakati huo huo, zipo taarifa kuwa huenda Kundi la muziki la vijana kutoka Uganda, Ghetto Kids, likashindwa kwenda kutumbuiza wakati wa hafla ya ufunguzi wa mashindano hayo.
Vijana hao wa Kampala walialikwa na staa wa muziki wa Pop, Shakira, kwa ajili ya kuimba naye jukwaani, ndoto ambayo sasa inaweza kupeperushwa na uwepo wa ugonjwa wa Ebola.
Katika kukabiliana na maambukizi, mamlaka za afya nchini Marekani zimetangaza utaratibu maalumu kwa wageni, hasa kipindi hiki cha Ebola na Kombe la Dunia.
Kwa utaratibu huo, kila mgeni atakayewasili akitokea DRC, Uganda au Sudan Kusini ndani ya siku 21 zilizopita, atapaswa kutumia viwanja vya ndege maalumu vya mjini Atlanta, New York au Washington.
Wakiwa hapo, wafanyiwa vipimo, kabla ya kuingia Marekani. Baada ya vipimo, mamlaka katika maeneo wanayokwenda kuishi zitajulishwa ili kufuatilia hali yao ya afya.
Endapo wageni watakutwa na maambukizi katika vipimo hivyo, upo utaratibu maalumu wa kuwapeleka katika hospitali zilizopangwa kwa ajili ya kuwapokea na kuwapa matibabu.
EBOLA NI NINI?
Ni ugonjwa unaosababishwa na virusi, ambavyo mara nyingi hushambulia wanyama, hasa popo. Binadamu hupata maambukizi kwa aidha kula au kuwa karibu na wanyama walioathirika.
Ebola huchukua siku mbili hadi 21 kwa dalili kuanza kuonekana, ambazo ni mafua, malaria, homa, koo kuwasha, maumivu ya misuli, macho kuwa mekundu, maumivu ya kichwa, na uchovu.
Baadaye, huanza kutapika, kuharisha, kutoka damu maeneo mbalimbali ya mwili, na hata baadhi ya viungo muhimu, zikiwamo maini, kushindwa kufanya kazi.
Virusi huhama kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mwingine kupitia vimiminika vya miwili, mathalan mate, damu au matapishi.
TOFAUTI YA EBOLA HII NA ZINGINE
Ebola ya safari hii inatokana na virusi aina ya Bundibugyo, hivyo ni tofauti na aina zingine mbili (Zaire na Sudan) za virusi vinavyosabaisha ugonjwa huo.
Tofauti na virusi vingine vya Ebola, Bundibugyo haina chanjo wala tiba. Kwamba wagonjwa wamekuwa wakipewa dawa kulingana na aina ya dalili walizonazo kwa wakati huo.
Mbaya zaidi katika kudhibiti maambukizi, mlipuko wa ugonjwa huo uko kwenye maeneo yenye vita nchini DRC, ambako watu wamekuwa wakihama kila muda, huku huduma za afya zikiwa hazipatikani kwa kiwango kizuri.


