9.5 C
New York

Mwangwi wa sheria| Polisi haihusiki na kesi hizi-2

Published:

WAKATI mwingine, kutokujua sehemu sahihi ya kupeleka malalamiko yako kunaweza kukupotezea muda, nguvu, na hata haki yako.

Mathalan, kwenda polisi kwa suala la madai ni kosa ambalo limekuwa likifanywa na walalamikaji wengi, bila kufahamu kuwa chombo hicho kinashughulika na makosa ya  jinai tu.

GAZETINI imefanya mahojiano na Wakili Baraka Asajile Gwakabake, ambaye anafafanua kwa kina namna kesi za madai zinavyoshughulikiwa, mahali sahihi ya kupeleka malalamiko na sheria zinazohukumu, endelea…

Mirathi, usimamizi wa mali za marehemu

Nani arithi, kwa kiasi gani, na nani hana haki. Ni Mahakama ndiyo huamua kwa kuzingatia uhalali wa mirathi. Polisi hawatoi urithi wala hawateui msimamizi wa mali.

Wakili Baraka anasema: “Mahali pa kwenda ni Mahakama ya Mwanzo, Wilaya, au Mahakama Kuu kulingana na thamani ya mali.

“Sheria zinazotumika ni Sheria ya Mirathi, Sheria ya Usimamizi wa Mirathi, Sheria za Kimila au Kiislamu pale inapohusika. Mirathi huamuliwa kwa nyaraka na sheria, si polisi au kwa kelele za familia.”

Madeni ya kibiashara au ya kawaida

Mtu amekukopa na hajalipa. Hili ni dai la madai, ambalo linahitaji uthibitisho na uamuzi wa Mahakama. Polisi hawalazimishi ulipaji wa deni bila amri ya Mahakama.

Anasema: “Mahali pa kwenda ni Mahakama ya Mwanzo au Mahakama ya Wilaya, Mahakama ya Hakimu mkazi, na mahakama kuu na Sheria inayotumika ni Sheria ya Mikataba. Deni halibadiliki kuwa kosa la jinai kwa sababu tu mtu hajalipa.”

Migogoro ya mikataba

Uvunjaji wa mkataba wa ujenzi, upangaji, mauziano, au huduma. Suluhisho ni madai ya kimahakama au usuluhishi. Polisi hawasimamii utekelezaji wa mikataba.

“Mahali pa kwenda ni Mahakama husika au Usuluhishi kama mkataba umeelekeza hivyo. Sheria inayotumika ni Sheria ya Mikataba. Mahakama huangalia makubaliano, masharti, na ukiukwaji wake,” anasema.

Migogoro ya wapangaji na wenye nyumba

Kodi, kufukuzwa, au marekebisho ya nyumba. Ni haki na wajibu wa kimkataba. Polisi hawatoi amri ya kufukuza mpangaji wala kumrudisha ndani ya nyumba.

Kwa mujibu wa Wakili Baraka, mahali anakopaswa kwenda mlalamikaji ni Baraza la Ardhi la kata na Sheria inayotumika ni Sheria ya Ardhi ya mwaka 1999.

Msomi huyo wa Sheria anasisitiza: “Hakuna kufukuza mpangaji kwa nguvu bila kufuata utaratibu wa kisheria.”

Migogoro ya ushirika wa kibiashara

Faida, hasara, mgawanyo wa mapato, au uongozi vinahitaji hesabu, mikataba, na ushahidi wa kimaandishi. Anasema:

“Polisi hawatatui mgogoro wa faida kwa maelezo ya mdomo. Faida na hasara hugawanywa kwa mujibu wa makubaliano, si kwa shinikizo.

“Hivyo, mahali pa kwenda ni Mahakama ya Biashara au Mahakama ya Wilaya. Sheria zinazotumika ni Sheria ya Majina ya biashara, Sheria ya makampuni na Sheria ya Mikataba.”

Madai ya fidia (Compensation)

Ajali, uzembe, au hasara ya mali. Kinachotafutwa ni fidia, si adhabu. Polisi hawahukumu kiasi cha fidia. “Mahali pa kwenda ni Mahakama ya Mwanzo au Wilaya au Hakimu Mkazi au Mahakama Kuu.

“Sheria zinazotumika ni Sheria ya Mwenendo wa Madai na Sheria ya Mikataba pale inapohusika. Lengo ni fidia na si adhabu,” anasema Wakili Baraka.

Migogoro ya ajira

Hapa tunazungunzia madai ya mishahara, kufukuzwa kazi na mafao. Napo kuna utaratibu maalumu wa kisheria unaoheshimu haki za pande zote (mwajiri na mwajiriwa).

“Polisi hawarudishi mtu kazini wala kuamuru mshahara ulipwe,” anasema Wakili Baraka na kuongeza:

“Mahali pa kwenda ni Tume ya Usuluhishi na Uamuzi wa Migogoro ya Kazi na Sheria zinazotumika ni Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini.”

Migogoro ya kifamilia isiyo ya jinai

Msaada wa mtoto, malezi, au makubaliano ya kifamilia. Hii Hutatuliwa kwa madai au usuluhishi, hivyo Polisi hawatatui haki za malezi kwa kufungana.

Anasema: “Mahali pa kwenda ni Baraza la Ustawi wa Jamii, Mahakama ya Mwanzo au Mahakama ya Wilaya. “Sheria inayotumika ni Sheria ya Mtoto. Masilahi ya mtoto ndiyo msingi, si hasira za wazazi.”

Mawasiliano: Wakili Baraka Asajile Gwakabake – 0784745645

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img