25.9 C
New York

Perez v Riquelme: Ni jeuri ya pesa, tambo za usajili mbio za urais Madrid

Published:

MADRID, Hispania

WANACHAMA takribani 700,000 wa klabu ya Real Madrid watapiga kura leo Juni 7, 2026 kuchagua Rais atakayeongoza kwa miaka minne ijayo.

Kwa sasa, vita ni kali kati ya Rais anayemaliza muda wake, Florentino Perez, na mwanachama mkongwe, Enrique Riquelme, ambapo wiki za hivi karibuni zimewashuhudia wakiendesha kampeni zao.

VITA YA MATAJIRI TU

Kuwania urais ndani ya klabu ya Madrid siyo rahisi kivile. Mbali ya kigezo cha uraia wa Hispania, pia mgombea anapaswa kuwa mwanachama wao kwa kipindi kisichopungua miaka 20.

Mbali ya hayo, lazima mgombea awasilishe ripoti ya fedha inayoonesha kuwa ana uwezo wa kumiliki asilimia 15 ya bajeti ya mwaka ya klabu.

Kwa sasa, bajeti ya mwaka ya Madrid ni Dola bilioni 1.16, hivyo mgombea urais awe na uwezo wa kumiliki asilimia 15 ya kiasi hicho. Kipengele hicho kiliwekwa katika maboresho ya Katiba ya mwaka 2012.

HUYU NDIYE PEREZ SASA

Perez (79), aliingia madarakani kwa mara ya kwanza mwaka 2000, ambapo aliifanya Madrid kuwa ‘chaka’ la wachezaji bora duniani alipowasajili Luis Figo, Zinedine Zidane na Ronaldo Nazario.

Mwaka 2006, kigogo huyo alijiuzulu, kabla ya kurejea madarakani mwaka 2009. Hata hivyo, hii ni mara yake ya kwanza kukutana na kigingi baada ya kupita bila kupingwa katika chaguzi zilizopita (2013, 2017 na 2021).

Ni rais mwenye mafanikio makubwa katika historia ya Madrid, ikiwamo kuufanyia marekebisho makubwa Uwanja wa Santiago Bernabeu, mataji saba ya Ulaya, saba ya La Liga, matatu ya Copa del Rey, na kuwa klabu tajiri zaidi duniani (Dola bilioni 9.5).

Kwa sasa, Perez anaungwa mkono na baadhi ya wakongwe wa Madrid, wakiwamo Gareth Bale, Roberto Carlos, Luka Modric na Karim Benzema.

Hata hivyo, amekumbana na ukosolewaji mkubwa katika siku za hivi karibuni baada ya Madrid kukosa taji kubwa lolote (Ligi ya Mabingwa na La Liga) kwa misimu miwili mfululizo iliyopita.

Katika baadhi ya mechi, mashabiki wamekuwa wakitumia nyimbo na hata mabango kumtumia ujumbe wa kutoridhishwa na kinachoendelea katika klabu yao hiyo.

Pia, mashabiki wamekuwa wakiwabebesha lawama wachezaji ghali waliosajiliwa, wakiwamo Kylian Mbappe na Jude Bellingham.

HUYU HAPA RIQUELME

Ni mfanyabiashara wa nishati na Mtendaji Mkuu wa kampuni ya Cox Group. Amejitosa kuutaka urais wa Madrid akiwa na umri wa miaka 37 tu.

Riquelme, licha ya kwamba aliwahi kumtaka Perez kuwa ndiye rais bora zaidi kuwahi kutokea Madrid, kwa sasa amekuwa akikosoa mambo makubwa mawili kwa kiongozi huyo.

Mosi, ukaribu wake na mfanyabiashara Anas Laghrari, ambaye si sehemu ya uongozi ndani ya Madrid lakini amekuwa akishirikishwa katika masuala mbalimbali, mathalan uboreshaji wa Santiago Bernabeu.

Pili, Riquelme anashangaa kuona Madrid, kwa mara ya kwanza katika historia, haina hata mchezaji mmoja kwenye kikosi cha timu ya Taifa ya Hispania kitakachokwenda Kombe la Dunia.

Wakati Perez akiahidi kumrejesha Jose Mourinho kwenye benchi la ufundi, Riquelme amekuja na jeuri yake, akisema atamchukua kocha wa zamani wa Liverpool, Jurgen Klopp.

Kama hiyo haitoshi, tajiri hiyo amedai kuwa endapo atachaguliwa, ataitikisa dunia kwa kuwasajili Erling Haaland na Rodri kutoka katika kikosi cha Manchester City.

Related articles

Recent articles