Na mwandishi wetu, Gazetini
MAJUKWAA ya kidigitali yamekuwa na faida kubwa kwa klabu za soka kuitangaza ‘brand’ yake, kama ilivyo muhimu kwa biashara zingine.
Aidha, si tu kujitangaza na kuwafikia mashabiki na wanachama katika kila kona ya dunia, bali pia mitandao ya kijamii imekuwa chanzo cha mapato kwa klabu nyingi.
Hii ni kutokana na fedha zinazotokana na matangazo ya kampuni mbalimbali zinazovutiwa kuweka bidhaa zake kwenye akaunti/kurasa za klabu zenye wafuasi wengi.
Kwa hapa nchini, Instagram na Facebook ni mitandao ya kijamii yenye ushawishi mkubwa, ikitumiwa na walau kila mtu anayemiliki ‘simu-janja’ (Smartphone).
Kwa upande wa soka la Bongo, vigogo Simba, Yanga na Azam nao wamekuwa wakitumia mitandao hiyo wa kampuni ya Meta ya Marekani. Takwimu zinaonesha kuwa vigogo hao ndiyo wenye wafuasi wengi Instagram na Facebook kuliko klabu zingine.
‘Wekundu wa Msimbazi’ ndiyo kinara kwenye eneo hilo kutokana na idadi yake ya wafuasi milioni nane, wakiziacha mbali Yanga na Azam.
Yanga, ambayo inashika nafasi ya pili, ina wafuasi milioni 4.8, ikizidiwa kwa takribani asilimia 50 ya idadi waliyonayo washindani wao wakubwa katika soka la Tanzania, Simba.
Katika nafasi ya tatu, ni Azam, ambayo ina wafuasi milioni 2.3, kwa maana ya nusu ya idadi ya Yanga na takribani mara nne ya wafuasi wa Simba.
Wakati huo huo, Simba inaongoza pia kwa ushawishi mkubwa katika mtandao wa kijamii wa Facebook ikiwa na wafuasi milioni tatu.
Kwa mujibu wa takwimu, idadi hiyo ni kubwa, ikilinganishwa na Yanga yenye wafuasi milioni 2.4 na Azam yenye milioni 1.1 huko Facebook.


