28 C
New York

Dunia haijasahau urafiki, uadui wa Dr. Dre, Eazy E

Published:

LOS ANGELES, Marekani

MOJA ya makundi yaliyoacha katika mapinduzi ya muziki wa Hip hop nchini Marekani na duniani kwa ujumla ni N.W.A lililoasisiwa mwishoni mwa miaka ya 1980.

Kundi lililoundwa mwaka 1978 na marapa Arabian Prince, Dr. Dre, Eazy-E, na Ice Cube, kabla ya DJ Yella na MC Ren kujiunga miezi michache baadaye.

Ushawishi wa Kundi hilo ulitokana na namna ngoma zao zilivyojikita katika kuzungumzia matatizo ya mtaani; ugumu wa maisha, uhalifu wa polisi na ubaguzi wa rangi dhidi ya watu weusi.

Kazi yao ya kwanza ikawa ni albamu maarufu ya ‘N.W.A. and the Posse’, ambayo ilivuma na kushika nafasi ya 39 katika chati za Billboard (R&B/Hip-Hop Albums).

Hata hivyo, albamu ya ‘Straight Outta Compton’ ya mwaka 1988 ndiyo iliyowatambulisha zaidi katika soko la muziki wa Marekani. Ikawa albamu ya kwanza ya wasanii weusi kuuza nakala nyingi zaidi Marekani na duniani.

Katika kilele cha ubora wao mwaka 1989, Kundi hilo lilitikiswa na hatua ya Ice Cube kujitoa. Alijiweka kando kwa kile kilichoelezwa wakati huo kwamba ni kutoridhishwa na mgawanyo wa fedha kwenye kundi.

Ice Cube aliingia kwenye ugomvi na aliyekuwa meneja wa Kundi, Jerry Heller, akidai kutokulipwa fedha alizostahili kwa kazi kubwa aliyoifanya ya kuandika ngoma nyingi katika Albamu yao ya Straight Outta Compton.

Pia, Ice Cube alidai malipo ya fedha zilizotokana na ushiriki wake katika kuandaa Albamu binafsi ya Eazy E iitwayo ‘Eazy-Duz-It’.

Kabla ya Ice Cube kuondoka, zilikuwepo taarifa zisizo rasmi kwamba meneja Heller alikuwa akimpendelea Eazy E kuliko wasanii wenzake wengine kwenye Kundi la N.W.A.

Akiwa msanii anayejitegemea (solo artist), Ice Cube aliachia albamu yake ya kwanza ya ‘AmeriKKKa’s Most Wanted’ mwaka 1990, wakati wenzake wa N.W.A. wakiachia EP yao ya ‘100 Miles and Runnin’.

Katika wimbo uliobeba jina la EP, kuna mstari unaosema: “Tulianza tukiwa watano lakini mmoja amezingua, sasa tuko wanne kwa sababu kundi la watu watano halikufanikiwa.” Hilo lilikuwa ni dongo kwa Ice Cube.

Taratibu, uadui wa Heller na Ice Cube ulianza kulihusisha kundi zima, hasa Eazy E, ambaye alikuwa karibu mno na meneja huyo.

Mwaka 1991, N.W.A. lilipitia mtikisiko mwingine. Kwa madai yala yake ya Ice Cube, Dr. Dre aliona meneja Heller anampendelea zaidi Eazy E. Uadui ukaanzia hapo.

Dr. Dre akaamua kujitoa na kuanza safari yake kama msanii wa kujitegemea. Ikawa ni vita kali kati yake na Eazy E, ikiwamo kutoleana lugha za matusi kupitia ngoma zao nyingi za mwanzoni mwa miaka ya 1990.

Februari, 1995, Eazy E alianza kuugua. Alipolazwa hospitali, alibainika kuwa na virusi vya Ukimwi. Mwezi mmoja tu baadaye, alijitangaza hadharani kuwa anaishi na ugonjwa huo, kisha alifariki siku 10 zilizofuata.

Akihojiwa mwaka 2015, Ice Cube alisema: “Nilikuwa naye (Eazy) miezi michache kabla ya kifo chake na tulizungumzia juu ya kurudi na kufanya kazi pamoja.

“Kipindi hicho, tulishamaliza tofauti zetu lakini yeye na Dre bado walikuwa na shida. Nikimwambia ‘kama utamwambia Dre, basi na mimi niko tayari’.”

Aidha, zipo taarifa kuwa Dr. Dre alifika hospitali wakati Eazy E akiwa amelazwa lakini hali aliyomkuta nayo haikumruhusu kuongea naye ili kumaliza tofauti zao.

Related articles

Recent articles