Na Hassan Mwasha
MAISHA ya Juma Mgota, mkazi wa Mtaa wa Muhalitan, Tandale jijini Dar es Salaam, yanaweza kuwa sehemu ndogo tu ya madhila wanayopitia vijana wengi walio kwenye urahibu wa dawa za kulevya ‘unga’.
Mgota (36), amebeba simulizi yenye kuumiza na hata majuto wakati mwingine, ambayo huenda vijana wengi walio kwenye matumizi ya unga wanayo na wanatembea nayo kwenye vifua vyao.
Watamwambia nani? Nani atawasilikiza? Jamii haipo upande wao tena, na badala yake imeelekeza nguvu zote kwa vijana wenzao wanaoonekana kuwa ‘smart’, werevu na majina mengine ya kutukuzwa.
GAZETINI imempa nafasi ya mahojiano kijana Mgota, mtoto wa kwanza kati ya watatu kwenye familia yao, akisimulia namna matumizi ya cocaine yalivyoharibu maisha yake na kuyafanya kuwa simulizi inayomuumiza.
Tofauti na vijana wengi wanaotaja ugumu wa maisha kama chanzo, Mgota ana simulizi ya aina yake, kwamba familia yake ilikuwa na uwezo mzuri tu wa kiuchumi.
Anasema: “Mungu alinijaalia kuzaliwa katika familia inayojiweza. Baba alikuwa na kipato kizuri kupitia biashara zake za kununua na kuuza mazao.
“Pale nyumbani, mimi na wadogo zangu, pamoja na mama yetu, tulipata huduma zote muhimu. Hata shule tulizosoma kuanzia chekechea, msingi hadi sekondari, hazikuwa hizi za Serikali. Tulisoma shule binafsi.”
CHANZO CHA TATIZO
Mgota, ambaye sasa ana miaka takribani mitatu tangu alipoachana na matumizi ya unga, anakumbuka alivyoingia kwenye janga hilo mwaka 2010 wakati huo akiwa amehitimu kidato cha nne na umri wake ukiwa ni miaka 18.
Anasema alianza kuvuta bangi na marafiki zake kwa kujificha, kabla ya kukutana na taarifa za upotoshaji zilizomuingiza moja kwa moja kwenye matumizi ya cocaine.
“Siku moja, tukiwa kwenye ‘geto’ la jamaa anayetuuzia bangi, alikuja kaka yake, ambaye kama nakumbuka vizuri alikuwa anaitwa Shebby na wakati huo alikuwa msanii chipukizi wa muziki.
“Sasa, katika stori zetu za hapa na pale, Shebby akaingizia kwamba cocaine inasaidia kumfanya mwanaume awe na nguvu za ziada anapokuwa faragha na mpenzi wake,” anasema Magota.
Taarifa hizo zilifungua ukurasa mpya katika maisha yake ya utumizi wa dawa za kulevya, ambapo Mgota aliachana kabisa na bangi na kuhamia kwenye cocaine.
“Mwanzoni, ilionekana kama ni kweli, lakini kadiri nilivyoendelea kutumia cocaine nilijikuta napoteza kabisa hamu ya kukutana kimwili na mwanamke.
“Ilifika kipindi nikawa naweza kukaa hata miaka mitatu bila kuwa na hamu na mwanamke. Kwa ufupi, iliniumiza kuona nimekuwa tofauti kabisa na vijana wa kiume wengine,” anasema.
KUIBA NYUMBANI, KUKIMBILIA SAUZI
Mwaka 2015, baada ya kufukuzwa nyumbani kutokana na matumizi ya unga yaliyokithiri, Magota alirejea kwa kisingizio cha kumuomba radhi baba yake, kana kwamba ameachana na mwenendo huo.
“Haikuwa hivyo. Kuna rafiki yangu alinishauri kwenda Afrika Kusini. Kumbuka, ni kipindi amabacho sikuwa na chochote, maana nisingeweza kuajirika kutokana na hali ya uteja niliyokuwa nayo.
“Kwa hiyo, kurudi kwangu nyumbani na kujifanya nataka kumuomba radhi baba ni kwa lengo la kupata nafasi ya kuiba chochote ambacho kingenipa fedha za nauli na kujikimu huko Sauzi.
“Kweli, baba alinipokea na nikaanza kuishi nao pale ‘home’. Wakati wote huo, akili yangu ilikuwa ni kupata cha kuiba. Kweli bwana, nikafanikiwa kuiba ‘tv’, nakumbuka ilikuwa inchi 32, redio kubwa, feni dogo, saa ya ukutani, na simu mbili,” anasema.
Hata hivyo, licha ya kupata takribani Shilingi 300,000, Magota anakiri kuwa maisha ya Afrika Kusini si rahisi kwa mtu yeyote, bali wale tu walioingia kwa mipango, kwa kufuata taratibu, na wenye ajira rasmi.
“Ukiacha kukosa uhuru kwa kuwindwa na polisi, maana tuliingia kwa njia za panya, ilikuwa ngumu hata kupata ajira. Nani ataajiri mateja, tena wasio na kibali cha kuishi?
“Tukajikuta tunaishi maisha magumu zaidi kuliko tulivyokuwa Bongo. Kukimbizana na polisi, kulala ufukweni au kwenye majengo mabovu, kushinda na kulala njaa,” anasema.
Wakati huo huo, Mgeto anakumbuka tukio la rafiki yake huyo kufariki mkononi mwake kwa kukosa huduma za afya kwa hofu ya kukamatwa na polisi endapo wangekwenda hospitali.
“Kama nilivyoeleza, tuliingia bila kufuata sheria, hivyo tulikuwa tunaishi kwa kujificha, tukihofia kukamatwa na polisi. Baada ya kifo chake mwaka 2023, nikaona huku (Sauzi) hakunifai. Nikarudi Tanzania,” anasema.
KUACHA UNGA, NENO KWA SERIKALI
Mgota anasema ugumu wa maisha aliyopitia Afrika Kusini, pamoja na kifo cha ‘mshikaji’ wake, vilimpa somo kubwa alipofika Tanzania na ndipo alipoamua kufungua na kuuanza ukurasa mpya.
“Haikuwa rahisi. Tofauti na wengine wanaotumia dawa za kuondosha uteja, niliacha mwenyewe. Tayari ilishaingia kwenye akili na moyo wangu, kwamba sasa dawa za kulevya hapana,” anasema.
Hata hivyo, anaongeza kuwa mwanzoni ushawishi wa kurudia unga ulikuwa mkubwa kutokana na marafiki zake wengi kuwa kwenye kundi hilo.
Anasema wakati mwingine alilazimika kuwakimbia ili kuepuka vishawishi. “Nashukuru Mungu, nikaanza kuzoea na wao pia wakaanza kunielewa, kwamba rafiki yao nimeamua kuchagua njia nyingine ya maisha.
“Nikawa sasa naweza kukaa nao kijiweni na kuwashauri kuachana na cocaine. Wapo walioelewa na sasa hwagusi kabisa,” anasema.
Hata hivyo, Mgota, ambaye kwa sasa ni mlinzi katika moja ya kampuni binafsi, anaiona changamoto kubwa kwa vijana wanaoamua kuachana na matumizi ya dawa za kulevya.
“Serikali ingetuwekea mfumo wa ajira vijana wa aina yetu. Unajua ukishatumia unga kwa miaka miwili tu, tayari unapoteza kila kitu, ikiwamo imani ya jamii kwako.
Mgeto anasema huenda vijana wengi wanatamani kuacha unga lakini wanakatishwa tamaa na namna walivyopitwa na fursa nyingi. “Wanajiona wameshaachwa mbali na vijana wenzao, ambao labda sasa ni wahasibu, madaktari, n.k.
“Kwa ushauri wangu, Serikali ituangalie kwa kutuwekea mazingira ya kiuchumi, hata kama tutakuwa tunapata posho badala ya mishahara. Hii itashawishi vijana wengi kuacha, wakiamini watapata nafasi nyingine ya kuendelea na maisha,” anasema.


