26.6 C
New York

Kombe la Dunia 2026: Harry Kane alivyobeba matumaini ya England

Published:

LONDON, Uingereza

KUFANIKIWA au kufeli kwa timu ya Taifa ya England ‘Three Lions’ katika fainali za Kombe la Dunia za mwaka huu (2026) kutategemea na kiwango cha straika wake, Harry Kane.

Mbali ya kuwa nahodha wa kikosi, Kane mwenye umri wa miaka 32 ndiye mfungaji bora wa muda wote wa timu hiyo (mabao 78 katika mechi 112).

Wakati huo huo, Kane anakwenda kwenye fainali hizo akiwa kwenye kiwango kikubwa, akifunga mabao 66 katika mechi 56 za Bundesliga msimu huu wa 2025-26.

Pia, Kane alifunga mabao yote katika ushindi wa mabao 3-0 wakati Bayern ilipoifunga Stuttgart na kutwaa ubingwa wa Kombe la Ligi nchini Ujerumani.

AMEIBEBA MABEGANI ENGLAND

Kwa mujibu wa straika wa zamani wa England, Chris Sutton, timu hiyo inapewa nafasi kubwa ya kufika mbali na hata kutwaa ubingwa msimu huu wa Kombe la Dunia kutokana na uwepo wa Kane kikosini.

“Harry Kane ni mchezaji muhimu kiasi kwamba kama leo hii atasema anastaafu timu ya taifa, basi nafasi yao ya kufanya vizuri haitokuwepo tena,” amesema Sutton.

Kwa upande wake, kipa wa zamani wa England, Paul Robinson, anasema licha ya kocha Thomas Tuchel kuwaita kikosini Ivan Toney na Ollie Watkins, pengo la Kane haliwezi kuzibwa na mchezaji yeyote.

Kane anakwenda Kombe la Dunia mwaka huu akiwa anashika nafasi ya pili, nyuma ya Gary Lineker, katika orodha ya wachezaji wa England wenye mabao mengi katika historia ya michuano hiyo.

Mshambuliaji wa kati huyo ana mabao nane katika mechi 11, wakati Lineker alistaafu akiwa amefunga mara10 kwenye michezo 12.

MKOSI WA EURO, KOMBE LA DUNIA

Licha ya mchango mkubwa alionao kikosini, Kane hajawa na bahati kwenye michuano mikubwa. Katika fainali za EURO 2016, hakufunga bao na England kuishia hatua ya 16 Bora.

Miaka miwili baadaye, England ilicheza Kombe la Dunia nchini Urusi na kuishia nusu fainali, licha ya Kane kuibuka mfungaji bora akiwa na mabao sita katika mechi sita.

Wakati wa michuano ya EURO 2020, alibeba tuzo ya mfungaji bora kwa mabao manne katika mechi saba lakini England yake ilifika fainali na kukosa ubingwa.

Mwaka 2022, wakati wa fainali za Kombe la Dunia nchini Qatar, England iliishia robo fainali, ambapo Kane akikosa penalti walipofungwa mabao 2-1 na Ufaransa katika mchezo wa robo fainali.

Tofauti kubwa ya Kane na washambuliaji wengine waliowahi kutokea katika historia ya soka la England ni mwendelezo wa kiwango kizuri.

Tangu alipoibuka na Tottenham msimu wa 2014-15, ambapo alifunga mabao 31 katika mechi 51, Kane amekuwa akifunga si chini ya mabao 24 kwa misimu 11 iliyofuata.

BORA KULIKO HAALAND?

Sutton, katika mahojiano yake ya hivi karibuni, amesema Kane ni straika bora kuliko Erling Haaland linapokuja suala la kufanya majukumu mengi kwenye eneo la mwisho.

“Unakumbuka Pep Guardiola alivyotaka kumsajili pale Manchester City? Unaweza kuona ni mabao mangapi angefunga kwa namna wanavyotengeneza nafasi.

“Ukiangalia idadi ya mabao aliyofunga tangu Haaland ajiunge na Man City, utaona kuwa Kane ni hatari zaidi mbele ya lango.

“Haaland ana kasi na nguvu lakini Kane yuko tofauti. Ni straika anayeweza kuchezesha wenzake kwenye eneo la mwisho,” amesema Sutton.

KUBEBA TUZO YA BALLON D’OR?

Amemaliza msimu huu wa 2025-26 akiwa ndiye mchezaji mwenye mabao mengi zaidi katika Ligi Kuu zote tano za Ulaya (England, La Liga, Bundesliga, Ligue 1 na Serie A).

“Atatwaa Ballon d’Or mwaka huu. Kama si yeye ni nani mwingine? Tazama idadi ya mabao aliyofunga katika ngazi ya klabu. Hakuna sababu ya kutoshinda tuzo. Kwa upande mwingine, ni yeye tu anayestahili kuitwaa,” amesema Sutton.

Hata hivyo, baada ya kulikosa taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya, ambapo Bayern iliishia nusu fainali, Sutton anaamini Kane atakuwa amejihakikishia Ballon d’Or endapo England itafanya vizuri msimu huu wa Kombe la Dunia.

Related articles

Recent articles