LONDON, Uingereza
Leighton ndiye anayewauzia magari mastaa wengi wa klabu. Miongoni mwao wachezaji aliochota fedha zao kwa kuwauzia ‘mandinga’ ya kifahari ni Harry Kane, John Terry, Kyle Walker na Paul Pogba.
Kama orodha hiyo haitoshi, pia wapo John Stones, Bruno Fernandes, Eberechi Eze, Leroy Sane, Georginio Wijnaldum na Pierre-Emerick Aubameyang.
Pia, Leighton aliwahi kufanya biashara ya pesa ndefu kwa kuwauzia magari Diogo Dalot, Viktor Gyokeres, Antony, Trevoh Chalobah na Yannick Bolasie.
Magari anayouza mshikaji hiyo ni yale ya kifahari, yakiwamo Ferraris, Lamborghini, Ford na hata Volkswagen Polo.
Kama itakumbukwa, wakati Antony akiwa mchezaji mpya katika klabu ya Manchester United, Leighton ndiye aliyemuuzia gari aina ya Lamborghini Aventador, ambapo alivuna Pauni 337,000.
“Dili nyingi ninazopata zinatokana na ‘koneksheni’ kutoka kwa wachezaji wenyewe. Wanagawana namba yangu ya simu. Wakati mwingine, mawakala wananipa bajeti au jina la gari, kisha nawatafutia linalofaa,” anasema.
Anasimulia alivyoanza biashara hiyo akisema alikuwa mwajiriwa wa moja ya kampuni za kuuza magari mjini Nottingham, England.
Hata hivyo, kwa sasa anamiliki kampuni yake inayofahamika kwa jina la Ultra Vita. Anasema: “Kwa sasa makubwa huru zaidi kufanya kile ninachokitaka. Dili zote nasimamia mwenyewe, majukumu yameongezeka.”
Ukiweka kando magari, pia kampuni yake hiyo inawauzia mastaa saa za bei mbaya, zikiwamo za Rolex zinazofanya vizuri kwa sasa kwenye soko la dunia.


