3.7 C
New York

Sangu: Wenye viwanda imarisheni afya na usalama wa wafanyakazi

Published:

Na Mwandishi Wetu, Gazetini

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu-Kazi, Ajira na Mahusiano, Deus Sangu, amewataka wamiliki wa viwanda na maeneo mengine ya kazi nchini kuzingatia kanuni bora za usalama na afya ili kulinda wafanyakazi wanaoshiriki katika uzalishaji viwandani.

Agizo hilo alilitolewa alipofanya ziara ya kufuatilia utekelezaji wa mifumo ya usalama na afya katika kiwanda cha kusindika samaki cha Omega Fish Limited, jijini Mwanza. Ziara hiyo ni sehemu ya mwendelezo wa ziara zake za kikazi za kutembelea taasisi na wadau mbalimbali wa sekta ya Kazi, Ajira na Mahusiano tangu alipochaguliwa kuiongoza wizara hiyo.

Waziri Sangu amesema kuwa ni jukumu la serikali kuhakikisha kwamba wafanyakazi wa taifa wanalindwa kikamilifu ili kutimiza malengo ya maendeleo, hususan utekelezaji wa Dira ya Taifa ya mwaka 2050. Pia, ameagiza Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) kushirikiana kwa karibu na wawekezaji katika kusimika mifumo madhubuti ya usalama na afya mahali pa kazi.

“Kanda ya Ziwa ina shughuli nyingi za kiuchumi. Ukiachilia mbali sekta ya uvuvi, OSHA imefanya kazi nzuri ya ukaguzi, lakini kuna sekta nyingine kama vile madini, ambapo baadhi ya migodi ya wazi inaanzishwa bila kufuata taratibu za usalama na afya,” amesema Waziri Sangu. Amesema:

“Hivyo, ninaiagiza OSHA kufanya ukaguzi wa kina katika maeneo yote ya kazi nchini, ikiwemo sekta ya madini, ili kuhakikisha kunakuwa na uzingatiaji wa taratibu zote muhimu za usalama na afya, jambo ambalo ni muhimu katika kulinda afya za watu na kuongeza tija katika uzalishaji.”

Awali, Katibu wa Jumuiya ya Viwanda vya Kusindika Samaki, Onesmo Sule, aliyehudhuria ziara ya Waziri, ameeleza changamoto zinazowakabili wasindikaji wa samaki nchini, zikiwemo upungufu wa malighafi unaosababishwa kwa kiasi kikubwa na uvuvi haramu, jambo linalosababisha viwanda kuzalisha chini ya uwezo wao na hivyo kuathiri ajira za Watanzania pamoja na kupoteza mapato ya kigeni.

Changamoto hiyo pia ilielezwa katika risala ya kiwanda cha Omega Fish Limited, iliyosomwa na Afisa Usimamizi wa Rasilimali Watu, Zena Marijan Juma, kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa kiwanda, Hamad Alsalman.

Akiongelea changamoto hizo, Waziri Sangu amesema Serikali imezipokea kwa uzito mkubwa na ameeleza kuwa zitashughulikiwa kwa ushirikiano na Wizara ya Mifugo na Uvuvi.

Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda, ambaye aliambatana na Waziri pamoja na watendaji wengine wa OSHA, amesema ziara hiyo ililenga kufuatilia utekelezaji wa sheria na kanuni za usalama na afya mahali pa kazi, kwa mujibu wa miongozo ya OSHA.

“Ziara hii ni sehemu ya utekelezaji wa majukumu yetu ya kila siku ya kufanya ukaguzi wa mifumo ya usalama na afya katika maeneo mbalimbali ya kazi. Kimsingi, tumeridhishwa na namna kiwanda hiki kinavyotekeleza miongozo tuliyokuwa tukiwapa mara kwa mara,” amesema.

Kiwanda cha Omega Fish Limited ni miongoni mwa viwanda 64 vya kusindika samaki nchini ambacho kinasindika samaki aina ya sangara na kuuza katika nchi mbalimbali za Ulaya na Asia.

Kwa mujibu wa takwimu za Wizara ya Mifugo na Uvuvi, uvuvi ni sekta muhimu katika maendeleo ya uchumi wa taifa. Katika mwaka 2023, sekta ya uvuvi ilichangia asilimia 1.7 katika Pato la Taifa (GDP) na kukua kwa asilimia 1.4. Aidha, sekta hii inatoa ajira kwa Watanzania takriban milioni 6, ikiwemo ajira za moja kwa moja kwa wavuvi wapatao 201,661 na wakuzaji viumbe wa majini 49,084 katika mnyororo wa thamani.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img