29.8 C
New York

Tanesco yapokea malori 214 kutoka Isuzu kuboresha huduma ya umeme nchini

Published:

na mwandishi wetu, Gazetini

SHIRIKA la Umeme Tanzania (TANESCO) limepokea malori 214 kutoka kampuni ya Isuzu East Africa kupitia Al Mansour Auto EA Tanzania kwa ajili ya kuimarisha shughuli za uendeshaji, matengenezo ya miundombinu ya umeme na kuongeza ufanisi wa utoaji wa huduma kwa wananchi nchini kote.

Akizungumza katika hafla ya makabidhiano iliyofanyika katika Ofisi za TANESCO, Ubungo jijini Dar es Salaam Ijumaa, Julai 10, 2026, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TANESCO, Mhandisi Timothy Mgaya, amesema malori hayo yatasambazwa katika mikoa na wilaya zote za TANESCO nchini ili kusaidia shughuli za ujenzi, ukarabati na matengenezo ya miundombinu ya umeme.

“Leo ni siku muhimu kwa TANESCO. Magari haya yatatusaidia kuboresha shughuli za uendeshaji na ukarabati wa miundombinu ya umeme ili kuhakikisha wateja wetu wanapata huduma ya uhakika, iliyo bora na endelevu,” amesema Mgaya.

Amesema ujio wa magari hayo unakwenda kupunguza changamoto ya upungufu wa magari ambayo kwa muda mrefu imekuwa ikiikabili TANESCO.

Mgaya amewataka madereva, mameneja wa wilaya na mikoa pamoja na watumishi wote watakaokabidhiwa magari hayo kuyatunza kwa kufuata ratiba za matengenezo ya kinga.

Sehemu ya magari hayo.

“Serikali kupitia TANESCO imewekeza takribani shilingi bilioni 66 kununua magari haya. Ni wajibu wetu kuyatunza vizuri ili yaendelee kuwahudumia wananchi na kuhakikisha huduma ya umeme haikatizwi,” amesema.

Awali, viongozi wa Isuzu East Africa wamesema ushirikiano kati ya kampuni hiyo na TANESCO ulianza mwaka 2022 kwa utoaji wa magari maalumu ya kreni, baadaye magari ya pikapu kwa ajili ya shughuli za kiutendaji, na sasa wamekabidhi malori 214 yenye uwezo wa tani 3 na tani 5.

Akizungumza kwa niaba ya Isuzu East Africa, Mkurugenzi wa mauzo wa Kanda, Kelvin Ochieng amesema viongozi wa kampuni hiyo amesema makabidhiano hayo yanaashiria kuimarika kwa ushirikiano kati ya pande hizo mbili na kwamba magati hayo yanafaa kwa mazingira ya Tanzania.

“Hatukuja leo kuanzisha ushirikiano na TANESCO, bali kuendeleza uhusiano ulioanza mwaka 2022. Ahadi yetu ni kuhakikisha magari haya yanapata huduma kwa wakati ili yaendelee kufanya kazi bila kusimama,” amesema.

Ameongeza kuwa Isuzu imejiandaa kutoa huduma baada ya mauzo kupitia vituo 27 vya huduma vilivyosambaa nchini, wahandisi wa matengenezo na magari maalumu ya huduma za dharura.

“Lengo letu ni kuhakikisha hakuna gari linalokwama kwa muda mrefu. Tunataka kuyawezesha magari haya kufanya kazi usiku na mchana ili kuisaidia TANESCO kufikisha huduma ya umeme kwa Watanzania wote,” amesema.

Related articles

Recent articles