24.1 C
New York

Uhaba wa mafuta wamfikisha pabaya Rais Putin

Published:

MOSCOW, Urusi

HALI ni mbaya mjini Moscow juu ya upatikanaji wa nishati ya mafuta. Foleni katika vituo vya mafuta (sheli) imeshuhudiwa kwenye maeneo mengi.

Mrundikano huo wa magari yanayosubiri huduma umechangiwa kwa kiasi kikubwa na uhaba wa petroli na dizeli nchini Urusi.

Inashangaza walio wengi kuona Urusi inapitia changamoto hiyo, licha ya kwamba ni moja ya nchi zenye utajiri na uzalishaji mkubwa wa nishati ya mafuta.

Hivyo, wananchi wengi wa Urusi wametupa lawama zao kwa Rais Vladimir Putin, wakisema vita kati yao na Ukraine vimechangia tatizo lililopo.

Katika vita hivyo vilivyodumu tangu mwaka 2022, Ukraine imekuwa ikitumia ndege zisizo na rubani kushambulia miradi ya usafishaji wa mafuta ya Urusi, ikiwamo iliyopo Moscow na St Petersburg.

Ni kutokana na uhaba wa mafuta unaowatesa wananchi kwa sasa, presha inarudi kwa Rais Putin kuhakikisha anakubali ombi alilolikataa kutoka kwa mwenzake wa Ukraine, Volodymyr Zelensky.

Zelensky alisema anataka kuona wanakaa mezani na kumaliza vita lakini Rais Putin aliweka wazi kuwa jambo hilo halitowezekana.

Lakini, kwa sasa presha ni kubwa zaidi kwa Rais Putin, ambapo tafiti zinaonesha kuwa ushawishi wake kwa raia umepungua na kubaki asilimia 74 pekee.

Pia, idadi ya wananchi wa Urusi wanaoamini kuwa Taifa lao linaelekea pazuri nayo imepungua kutoka asilimia 61 hadi asilimia 52, kwa mujibu wa utafiti wa Taasisi ya Levada.

Je, ikizingatiwa kuwa uhaba wa mafuta una athari za moja kwa moja kwa uchumi wa Urusi, Rais Putin atakubali kukaa mezani na Zelensky ili kumaliza vita vya miaka minne sasa?

Related articles

Recent articles