38.3 C
New York

JET: Asasi za kiraia ni nguzo ya kupambana na jangwa

Published:

Na mwandishi wetu, Gazetini

MKURUGENZI Mtendaji wa Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira Tanzania (JET), John Chikomo, amesema asasi za kiraia zina nafasi muhimu katika kukabiliana na kuenea kwa jangwa nchini kupitia utoaji wa elimu kwa umma, utetezi wa sera, kujenga uwezo wa jamii na kushirikiana na Serikali katika usimamizi endelevu wa ardhi.

Chikomo ametoa kauli hiyo alipowasilisha mada yenye kichwa”Nafasi ya Asasi za Kiraia katika Kukabiliana na Kuenea kwa Jangwa Tanzania” wakati wa Warsha ya Kitaifa ya Maandalizi ya Mkutano wa 17 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Kupambana na Kuenea kwa Jangwa (UNCCD COP17), iliyofanyika Juni 30, 2026, jijini Dodoma.

Warsha hiyo iliandaliwa kupitia Mradi wa Kilimo Endelevu Arusha (KEA), unaotekelezwa na MVIWAARUSHA, CARI na RECODA kwa ufadhili wa Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD), ikiwa na lengo la kuimarisha ushiriki wa wadau wa Tanzania katika maandalizi ya mkutano wa UNCCD COP17 utakaofanyika Ulaanbaatar, Mongolia, kuanzia Agosti 17 hadi 28, 2026.

Akiwasilisha mada yake, Chikomo amesema JET imeendelea kutumia uandishi wa habari za mazingira kama nyenzo ya kuhamasisha jamii kulinda mazingira, kupambana na uharibifu wa ardhi na kuongeza uelewa kuhusu athari za mabadiliko ya tabianchi pamoja na matumizi endelevu ya rasilimali za asili.

Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira Tanzania (JET), John Chikomo.

Aidha, amesema JET itaendelea kuiwakilisha Tanzania katika majukwaa ya kimataifa, ikiwemo mkutano wa UNCCD COP17, kwa lengo la kuhakikisha sauti za jamii na wadau wa mazingira zinazingatiwa katika mijadala na maamuzi yanayohusu uhifadhi wa ardhi duniani.

“Asasi za kiraia ni daraja muhimu kati ya jamii, Serikali na wadau wa maendeleo katika kuhakikisha juhudi za kukabiliana na kuenea kwa jangwa zinakuwa shirikishi na zenye matokeo endelevu,” amesema Chikomo.

Alisema pamoja na kuhamasisha jamii, asasi za kiraia zina mchango mkubwa katika kutekeleza miradi ya uhifadhi wa mazingira, kujenga uwezo wa wananchi, kutetea sera zinazolinda mifumo ikolojia iliyo hatarini na kuhimiza usimamizi wa haki wa rasilimali za asili.

Ameongeza kuwa asasi hizo pia zinaendelea kushirikiana na Serikali katika utekelezaji wa Mpango wa Kitaifa wa Kukabiliana na Kuenea kwa Jangwa (National Action Programme – NAP), unaoendana na Mkataba wa UNCCD, kwa lengo la kufikia azma ya kutokomeza uharibifu wa ardhi (Land Degradation Neutrality – LDN) ifikapo mwaka 2030.

Kwa mujibu wa waandaaji, warsha hiyo ililenga kuwajengea uwezo wadau kuhusu mchakato wa UNCCD, kubadilishana uzoefu kuhusu usimamizi endelevu wa ardhi, kujadili matokeo ya Désertif’actions 2026 na kuandaa mapendekezo ya Tanzania yatakayowasilishwa katika mkutano wa COP17.

Warsha hiyo iliwakutanisha wawakilishi wa Serikali, asasi za kiraia, taasisi za utafiti na mashirika ya maendeleo yanayojihusisha na usimamizi endelevu wa ardhi, urejeshaji wa maeneo yaliyoharibiwa, kilimo ikolojia na kuimarisha ustahimilivu dhidi ya mabadiliko ya tabianchi.

Akifungua warsha hiyo, mwakilishi wa Kitengo cha Kitaifa cha Mkataba wa UNCCD kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais- Idara ya Mazingira, Abdallah Lungo, amesisitiza umuhimu wa ushirikiano wa wadau wote katika kuandaa msimamo wa Tanzania kuelekea COP17 ili kuimarisha mchango wa nchi katika juhudi za kimataifa za kupambana na kuenea kwa jangwa na kurejesha afya ya ardhi.

Related articles

Recent articles