Na mwandishi wetu, Gazetini
CHAMA cha Waandishi wa Habari za Mazingira Tanzania (JET) kimetoa wito kwa jamii, Serikali na wadau mbalimbali kuongeza kasi ya hatua za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi huku kikionya kuwa dunia tayari inaonyesha dalili hatari za uharibifu wa mazingira.
Katika ujumbe wake kuelekea Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani (WED) 2026 yatakayofanyika Juni 5, JET imesema ongezeko la kina cha bahari, mawimbi ya joto, kuyeyuka kwa barafu, moto wa nyika na uchafuzi wa mazingira ni ishara zinazoonyesha dunia ipo katika kipindi kigumu cha mabadiliko ya tabianchi.
“Sayari haitoi hoja wala kujadiliana, bali inatuma ishara,” amesema Mkurugenzi Mtendaji wa JET, John Chikomo, katika taarifa iliyotolewa Dar es Salaam leo, Juni 4, 2026.
Kaulimbiu ya maadhimisho ya mwaka huu duniani ni “Iliongozwa na asili. Kwa hali ya hewa. Kwa wakati ujao wetu,” inayolenga kuhimiza matumizi ya nishati safi, urejeshaji wa mifumo ikolojia na ushirikiano wa kimataifa katika kulinda mazingira.
JET imesisitiza kuwa waandishi wa habari za mazingira wana wajibu mkubwa wa kuendelea kuhabarisha jamii kuhusu athari za mabadiliko ya tabianchi na umuhimu wa kuchukua hatua za uhifadhi wa mazingira.
Kitaifa, kilele cha maadhimisho hayo kitafanyika jijini Dodoma chini ya kaulimbiu isemayo “Dira 2050, Tuwajibike Kukijanisha Tanzania,” inayolenga kuhamasisha uwajibikaji wa jamii katika usimamizi wa mazingira.
“Ni kwa ajili yangu, ni kwa ajili yako, ni kwa ajili yetu sote – chukua hatua leo, hata kama ni ndogo,” amesema Chikomo.


