27.2 C
New York

Karim Khan: Kuigusa Israel kumemfukuzisha kazi ICC?

Published:

Na mwandishi wetu, Gazetini

HATIMAYE Karim Khan ameondoshwa katika kiti cha Mwendesha Mashitaka Mkuu wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC). Kashfa ya unyanyasaji wa kingono ndiyo iliyomng’oa kwenye kiti hicho.

Kwamba Khan alimnyanyasa kingono, ikiwamo kumshika bila ridhaa yake mfanyakazi wa kike, ambaye alikuwa msaididi wake kwenye ofisi hiyo ya Mwendesha Mashitaka.

Hatua ya kuondoshwa kwenye nafasi hiyo ni matokeo ya kura zilizopigwa na wanachama wa ICC katika Mkutano wa hivi karibuni uliofanyika Makao Makuu ya mjini New York.

Khan raia wa Uingereza, alichaguliwa mwaka 2021 na ni Mwendesha Mashitaka wa tatu katika historia ya ICC.

MCHAKATO WA KUMNG’OA

Madai ya Khan kumdhalilisha kingono msaidizi wake, Sarah, yaliibuka kwa mara ya kwanza Mei, 2024.

Chombo huru ndani ya ICC (IOM) kilianza uchunguzi wake lakini kesi ilifungwa hapo baadaye baada ya Sarah kukataa kutoa ushirikiano.

Vilevile, uchunguzi wa IOM ulibaini kuwa hakukuwa na ushahidi wa kutosha kuthibitisha Khan alifanya unyanyasaji huo.

Miezi mitano baadaye, kesi hiyo ilifufuka, safari hii ikipelekwa Umoja wa Mataifa na uchunguzi kufanywa na chombo chake cha OIOS.

Ndipo OIOS ilipofanya uchunguzi wake kuanzia Novemba, 2024, hadi Desemba, 2025, na kuja na ripoti ya ushahidi yenye kurasa zaidi ya 5,000.

Hata hivyo, licha ya ripoti ya uchunguzi kuja na ushahidi, ilihitaji kura walau 63 kati ya nchi wanachama 125, sawa na asilimia 50.4, zinazounga mkono uamuzi wa Khan kufutwa kazi.

Kura hizo zilipigwa Julai 24, 2026, na idadi ilipotimia (82) ndipo ICC ilipotangaza rasmi kuwa Khan ameondoshwa kwenye nafasi yake.

KHAN ANASEMAJE?

Khan amekana mara zote kuhusika katika unyanyaji wa kingono dhidi ya mwanamke huyo aliyetajwa kwa jina moja la Sarah.

Mwanasheria wake, Sareta Ashraph, pia anasema mteja wake hakuwahi kumgusa au kuwa na uhusiano wa kimapenzi na mwanamke huyo.

Pia, Ashraph anasema Khan alipaswa kupewa haki ya kujitetea wakati wa mchakato wa upigaji kura lakini hakuweza kwenda Marekani kutokana na vikwazo alivyowekewa na nchi hiyo.

“Tunafahamu kuwa hakuna mfumo wa kisheria unaomzuia mtu mwenye mashitaka kusikilizwa,” alisema Tayab Ali, ambaye pia ni mwanasheria wa Khan.

Kwa sasa, Khan ambaye ni mwanasheria raia wa Uingereza, haruhusiwi kuendelea na taaluma hiyo nchini humo hadi Bodi ya Wanasheria itakapokamilisha uchunguzi wake juu ya shutuma hizo.

KESI YA KISIASA?

Wapo wanaoamini kuwa mashitaka dhidi ya Khan, kisha kufukuzwa kazi, ni matokeo ya hatua ya ofisi yake juu ya mgogoro wa Gaza kati ya Israel na Palestina.

Khan aliongoza chunguzi za uhalifu wa kivita dhidi ya Israel, ikifikia hatua ya kutoa kibali cha kukamatwa kwa Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, na Waziri wake wa Ulinzi wakati huo, Yoav Gallant.

Licha ya kwamba Israel si mwanachama wa ICC, kama zilivyo Marekani na Urusi, inaweza kumfungulia mashitaka kiongozi wa nchi yoyote kati ya hizo endapo nchi yake itafanya uhalifu kwa mwanachama wake. Palestina ni mwanachama wa ICC.

Hatua yake hiyo ndiyo iliyosababisha Marekani kumwekea Khan na viongozi wengine wa ICC kikwazo cha kuingia nchini humo.

“Siasa zimeingia hapa, ikizingatiwa kuwa ni mara ya kwanza kwa mwendesha mashitaka kutoa kibali cha mshirika kwa Magharibi (Iran) kukamatwa,” amesema Iva Vukusic, mtafiti wa Chuo Kikuu cha Utrecht.

Naye mwanadiplomasia wa zamani wa Umoja wa Ulaya (EU), Josep Borrell, amesema mashitaka dhidi ya Khan ni mwendelezo wa ICC kuingiliwa.

Kwa kile kilichomkuta Khan, wengine wanahisi kwamba ICC inawekwa kwenye mazingira ya kuziogopa nchi kubwa hata pale zinapoingia kwenye uhalifu wa kivita au uhalifu dhidi ya binadamu.

Wakati huo huo, taasisi mbalimbali za haki za binadamu za Palestina zimelaani kilichotokea kwa Khan, zikieleza kuwa siasa chafu dhidi yake, hasa baada ya kutaka Netanyahu akamatwe, ndiyo chanzo cha mashitaka.

Hata hivyo, Sarah ambaye ndiye aliyeibua madai ya kudhalilishwa kingono na Khan, amekana siasa kuhusika, akisema hajatumwa na Israel wala taifa lolote kumchafua.

Related articles

Recent articles