27.2 C
New York

Rais wa Senegal azindua chama chake

Published:

DAKAR, Senegal

RAIS wa Senegal, Bassirou Diomaye Faye, amezindua chama kipya cha kisiasa kiitwacho Kiiray (Chama cha Wazalendo wa Jamhuri), hatua inayotajwa kuimarisha mgawanyiko wa kisiasa kati yake na mshirika wake wa zamani, Ousmane Sonko.

Uzinduzi huo ulifanyika jijini Dakar siku ya Jumamosi ukihudhuriwa na mamia ya wafuasi wa rais. Wakati huohuo, Sonko alikuwa akizungumza na wafuasi wake katika mji wa Bambey, ikiwa ni sehemu ya ziara ya kitaifa ya kuimarisha chama chake cha Pastef.

Mapema mwezi huu, Rais Faye alimteua mshauri wake mkuu, Aminata Touré, kuongoza mchakato wa kuanzisha chama hicho kipya. Kabla ya kuwa rais, Faye alikuwa Katibu Mkuu wa Pastef, chama kilichoshinda uchaguzi wa mwaka 2024 baada ya miaka mingi ya kuwa upinzani.

Hata hivyo, uhusiano kati ya Faye na Sonko umeendelea kuzorota katika miezi ya karibuni na kufikia kilele mwezi Mei baada ya Faye kumwondoa Sonko katika nafasi ya Waziri Mkuu. Sonko kwa sasa ni Spika wa Bunge la Kitaifa.

Uzinduzi wa Kiiray unafanyika wakati viongozi na wanachama kadhaa wa Pastef wakihamia kambi ya rais, hali inayokipa chama hicho changamoto ya kudhibiti wimbi la wanachama wanaokihama.

Wachambuzi wanaeleza kuwa mgawanyiko huo unaashiria mabadiliko makubwa katika siasa za Senegal kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa wa mwaka 2027, huku viongozi hao wawili wakiongoza kambi tofauti zinazowania ushawishi wa kisiasa nchini humo.

Related articles

Recent articles