27.2 C
New York

Rais Trump na maswali yanayokosa majibu kuhusu Iran

Published:

TEHRAN, Iran

VITA vinaendelea. Si Marekani wala Iran, kila upande umekiuka makubaliano ya kusitisha vita yaliyoingiwa na pande mbili hizo wiki chache zilizopita.

Wakati vita vinaanza Februari 28,2026, Wamarekani na washirika wao, Israel, waliamini na hata kudai kuwa ingewachukua muda mfupi tu kumaliza kazi. Ni miezi mitano sasa.

Kwa upande mwingine, Rais Trump amekuwa akiibua madai ambayo kadiri siku zinavyozidi kwenda, yanathibitika kuwa hayana ukweli.

Mosi, aliwahi kusema wameshaimaliza Iran. Machi, 2026, Rais huyo alisema: “Tumemaliza kila kitu, ikiwamo uongozi wao. Hawawezi tena kupigana.”

Mei, 2026, kiongozi huyo akaibuka na madai mengine, akisema: “Jeshi la Iran limekwisha. Tumeshalimaliza jeshi lao.”

Kauli hizo na nyingine ya aina hiyo aliyoitoa mwanzoni mwa Julai, 2026, haiendani na uhalisi. Jeshi la Iran limeendelea kufanya mashambulizi, hasa dhidi ya nchi za Mashariki ya Kati zenye urafiki na Marekani. Mbaya zaidi, vimeshuhudiwa pia vifo kadhaa vya wanajeshi wa Marekani katika mashambulizi hayo.

Hata kabla ya mashambulizi hayo, tayari kituo kikubwa cha televisheni cha CNN kilisharipoti kuwa majasusi wa Marekani wamebaini kwamba Iran bado ina nguvu kubwa ya kijeshi, tofauti na madai ya Rais Trump.

Wakati fulani, ilitokea mara kadhaa Rais Trump kujikanyaga kwa kusema Iran bado ina makombora na ndege zisizo na rubani, licha ya uharibifu mkubwa uliofanywa na Marekani.

Pili, ni ishu ya muda wa vita. Mwanzoni mwa mashambulizi ya Marekani dhidi ya Iran, Rais Trump aliiahidi dunia kuwa wangetumia muda mfupi tu kuituliza Iran.

“Ni takribani wiki nne tu. Kwa ukubwa na uimara wa nchi yenyewe, itatuchukua wiki nne (kuisambaratisha) au chini ya hapo,” alisema Rais Trump.

Muda alioahidi umepita. Ni miezi takribani mitano sasa ya vita na hakuna dalili ya Iran kuweka silaha chini au kusambaratishwa kama alivyodai Rais Trump.

Tatu, ni ishu ya Mlango-Bahari wa Hormuz. Julai 13, 2026, Rais Trump aliposti mitandaoni kuwa njia hiyo inayosafirisha asilimia 20 ya mafuta na gesi asilia kuingia soko la dunia iko wazi na haiko tena chini ya udhibiti wa Iran.

Rais Trump alienda mbali zaidi na kusema kwa sasa Hormuz inalindwa na wanajeshi wa Marekani ili kuzihakikishia usalama meli zinazopita dhidi ya mashambulizi ya Iran.

“Ndiyo, tunaishikilia Hormuz. (Iran) haina tena udhibiti. Tunaidhiti Hormuz. Iran hawana wanachodhibiti kwa sasa,” alisema Rais huyo.

Tofauti na madai yake hayo, Iran imeendelea kudhibiti Hormuz, huku Marekani ikikimbilia kuzuia meli za mafuta zinazoingia na kutoka katika bandari za nchi hiyo ya Kiarabu.

Kwamba hadi sasa Iran imeendelea kuzishambulia meli zote zinazopita Hormuz bila kufuata taratibu zake.

Nne, ni ishu ya bei ya mafuta. Juni, 2026, ni kweli bei ilishuka baada ya Marekani na Iran kukubaliana kusitisha vita. Julai 8, 2026, Rais Trump aliibuka na kusema bei itashuka zaidi na kurudi kama ilivyokuwa kabla ya vita.

Hata hivyo, ahadi hiyo haionekani kutimia. Bei ya nishati hiyo imerudi juu, hasa baada ya pande mbili hizo kukiuka makubaliano ya kusitisha vita kwa siku 60 ili kupisha mazungumzo.

Kwamba bei ya mafuta ghafi kwenye soko la dunia imepanda si tu kuliko ilivyokuwa kabla ya vita, bali kuliko kipindi chote cha awamu yake ya pili madarakani.

Hivi karibuni, licha ya kuona kabisa kuwa vita bado ni mbichi, Rais Trump alitoa ahadi ile ile, kwamba bei ya mafuta itashuka, akiwamba Wamarekani wampe muda kidogo tu.

Related articles

Recent articles