31.4 C
New York

Vijana 100 wasonga mbele Vijana Uchumi Challenge 2026

Published:

Na Ramadhan Hassan, Dodoma

KAMATI ya Kitaifa ya Shindano la Vijana Uchumi Challenge imetangaza rasmi majina ya vijana 100 bora waliofanikiwa kuingia hatua inayofuata ya mashindano hayo baada ya mchakato mkali wa ushindani ulioshirikisha maombi 7,852 kutoka mikoa yote nchini.

Hayo yameelezwa Juni 5, 2026 na  Katibu wa Kamati ya Kitaifa ya Vijana Uchumi Challenge, Amina Sanga wakati alipokuwa akizungumza na Waandishi wa Habari Jijini hapa.

Amesema  shindano hilo ni sehemu ya utekelezaji wa maono ya Serikali ya Awamu ya Sita pamoja na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 kwa kuwapa vijana fursa ya kushiriki kikamilifu katika kukuza uchumi wa nchi.

Sanga amesema  dirisha la kupokea mawazo ya vijana lilifunguliwa Aprili 13, 2026 na kufungwa Mei 7, 2026, ambapo jumla ya maombi 7,852 yalipokelewa kutoka maeneo mbalimbali nchini.

Amesema kati ya maombi hayo, mawazo 458 yalipata alama za juu na kuwasilishwa katika hatua ya mwisho ya uchambuzi kabla ya kupatikana kwa washiriki 100 bora waliotangazwa rasmi

“Vijana hawa 100 bora wataingia katika kambi maalumu ya mafunzo ya siku nne ambayo itawalenga kuwajengea uwezo wa kuboresha mawazo yao, kuyafanya yaweze kutekelezeka zaidi na kuwapa stadi za kuyawasilisha mbele ya majaji, wawekezaji na wadau mbalimbali wa maendeleo,” amesema  Sanga.

Kutokana na mwitikio mkubwa wa vijana na ubora wa mawazo yaliyowasilishwa, Kamati ya Kitaifa ya mashindano hayo imetangaza kuongeza thamani ya zawadi zinazotolewa kwa washindi.

Kwa mujibu wa kamati hiyo, mshindi wa kwanza sasa atajishindia Sh milioni 50 badala ya Sh milioni 30 zilizokuwa zimetangazwa hapo awali.

Alisema mshindi wa pili atapata Sh milioni 30 huku mshindi wa tatu akizawadiwa Sh milioni 20. Aidha, washiriki watakaoshika nafasi ya nne hadi ya kumi watapatiwa Sh milioni tatu kila mmoja kama sehemu ya kutambua mchango wao katika kuibua mawazo ya ubunifu yatakayosaidia maendeleo ya taifa.

Related articles

Recent articles