Na mwandishi wetu, Gazetini
HATIMAYE bei ya mafuta ya petroli imeshuka wa Shilingi 29 kwa Dar es Salaam, ambapo sasa lita moja itauzwa kwa Shilingi 4,086 kutoka Shilingi 4,115.
Wakati huo huo, bado hali ni tete kwa upande wa dizeli, ambapo bei imepanda kwa Shilingi 85 kwa lita na kufikia Shilingi 4,333 kutoka bei ya awali ya Shilingi 4,248.
Bei hizo zitaanza kutumika leo Juni 3, 2026, kwa mujibu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA).
Katika taarifa yake iliyotolewa na Kaimu Mkurugenzi Mkuu, Gerald Maganga, EWURA imeeleza kuwa mabadiliko hayo yametokana na mgogoro wa Mashariki ya Kati.
Ifahamike kuwa eneo hilo limekuwa kwenye vita tangu Februari 28, 2026, ambapo Marekani kwa kushirikiana na Israel zimekuwa zikikabiliana na Iran.
“Tanzania inaagiza sehemu kubwa ya mafuta yake kutoka nchi za Mashariki ya Kati, hivyo athari za mabadiliko hayo ya kimataifa zimejitokeza moja kwa moja katika soko la ndani,” amesema Maganga.
Katika hatua nyingine, Maganga amesema Serikali imechukua hatua katika kupunguza makali yatokanayo na vita hivyo vinavyoathiri bei ya nishati ya mafuta katika soko la dunia.
Amesema: “Miongoni mwa hatua hizo ni utoaji wa ruzuku ya takriban Shilingi 534.91 kwa kila lita moja ya mafuta ya dizeli.
“Dizeli ni muhimu katika shughuli za kiuchumi na kijamii zikiwemo uzalishaji viwandani, usafirishaji wa bidhaa na huduma za usafiri wa umma,” amesema.”
Wakati huo huo, amesema bei ya mafuta ya taa yanayopita Bandari ya Dar es Salaam nayo imepanda kwa Shilingi 85, hivyo sasa yatanunuliwa kwa Shilingi 4,685 badala ya Shilingi 4,677.
“Kwa upande wa watumiaji wa petroli inayopitia katika Bandari ya Tanga, lita moja itauzwa kwa Shilingi 4,157 kutoka Shilingi 4,176, ikiwa ni ongezeko la Shilingi 19 kwa kila lita.
“Wanaotumia mafuta ya dizeli yanayopita katika bandari hiyo sasa watanunua lita moja kwa Shilingi 44,04 kutoka Shilingi 4,309, ikiwa ni ongezekoo la Shilingi 95 kwa lita,” amesema Maganga.


