LAGOS, Nigeria
SUPASTAA wa muziki wa Afrobeats, David Adeleke, maarufu Davido, amekiri kuwa wasanii, akiwamo yeye, hawajafanya vya kutosha kusimama na wananchi katika changamoto zinazowakabili.
Wakati huo huo, Davido ameweka wazi kuwa yeye si mfuasi wa chama chochote cha siasa, na angependa wasanii wengine wawe hivyo.
“Siwezi kudanganya, sisi waburudishaji tunazingua, nikiwamo mimi. Tunapaswa kupaza sauti. Kuna shida nyingi zinazoendelea. Nchi yetu inapotea,” alisema.
Kwa miaka mingi ya hivi karibuni, imekuwapo mijadala mingi juu ya nafasi ya wasanii katika jamii, hasa linapokuja suala la kutokujihusisha na wanasiasa, na badala yake kusimama na wananchi.
Hata hivyo, sababu za kiuchumi na hofu ya kudhuriwa zimekuwa zikitajwa kuwafanya wasanii kuchagua upande wa wanasiasa, na kuacha jukumu la msingi la kusimama na jamii.


