NAIROBI, Kenya
MUONGO mmoja uliopita, Jumuhiya ya Afrika Mashariki (EAC), ilikiri kuwapo kwa utitiri wa nguo za mitumba na kutangaza mkakati wa kuweka mazingira magumu ya uingiaji wake katika nchi zake.
Nchi sita za EAC wakati huo – Burundi, Kenya, Rwanda, Sudan ya Kusini, Tanzania na Uganda – zilitangaza kuwa zingeweka ushuru mkubwa kwa nguo hizo zilizotumika.
Lakini, Marekani, ambayo ndiyo msafirishaji mkubwa wa mitumba barani Afrika, iligomea hatua hiyo, ikidai kuwa inakinzanana na mkataba wa kimataifa wa Ukuaji na Fursa barani Afrika (Agoa).
Baada ya shinikizo la Marekani, pendekezo hilo lilipigwa chini, ingawa bado umekuwapo mjadala mkubwa juu ya mitumba zinavyoathiri soko la nguo za ndani.
Kwa mujibu wa takwimu za Taasisi ya Masuala ya Kiuchumi ya OEC (Observatory of Economic Complexity), Kenya inaongoza kwa uagizaji wa mitumba kwa Ukanda wa Afrika Mashariki.
Mzigo wa mitumba wa tani takribani 180,000 iliingia nchini humo mwaka 2022, likiwa ni ongezeko la asilimia 76, ikilinganishwa na takwimu za mwaka 2013, inaeleza ripoti ya Umoja wa Mataifa (UN).
Licha ya kushindwa kuzuia kabisa uingizwaji wa mitumba, Kenya, kama ilivyo kwa Rwanda, nazo zimepandisha kwa asilimia 30 ushuru wa nguo hizo zilizotumika.
Uganda, kwa upande wake, imetambulisha ongezeko la asilimia 30 ya kodi ya nguo hizo zinazoingia Afrika baada ya kutumika katika mataifa ya Ulaya, Asia na Marekani.
Kama ilivyo kwa Kenya, Uganda nako mitumba inaongoza, ikifuatiwa na nguo mpya zinazotoka nje, kisha zile zinazozalishwa ndani, kwa mujibu wa Kituo cha Taifa cha Utafiti wa Sera za Kiuchumi.
Katika kudhibiti uingiaji wa mitumba, Serikali ya Uganda imeweka imeweka ushuru wa asilimia 30. “Lengo ni kupunguza uingiaji wa mitumba na kulipa thamani soko la nguo zinazotengenezwa nchini,” inaeleza Ripoti ya chombo cha habari cha Uganda, Kampala Report.
Kwa upande wa majirani zao, Tanzania, ushuru wa uagizaji wa nguo za mitumba ni asilimia 35, ingawa bado ni kimbilio la wananchi walio wengi.
Aidha, mtaalamu wa uchumi, Dkt. Andrew Brooks, haoni tija ya mitumba katika sekta ya uchumi wa nchi. Na badala yake, anasisisitiza uchumi unaohusisha uzalishaji, masoko na usambazaji.
Je, ni zipi changamoto za kudhibiti nguo za mitumba? Serikali za Afrika Mashariki zinaweza kuwa na mikakati mingi ya kuzuia mitumba katika nchi zake, lakini zipo chagamoto kadhaa, ikiwamo ya shinikizo la Marekani, ambayo ni muuzaji kinara wa nguo hizo kwa nchi za Afrika.
Kwa kuruhusu mitumba kuingia, nchi hizo hupata faida ya kuondoshewa ushuru katika baadhi ya bidhaa zake zinazokwenda Marekani.
Pili, nguo hizo ni kimbilio la wananchi wake kutokakana na unafuu wa bei. Watumiaji nchini Kenya ni takribani milioni 4.9, kwa mujibu wa Chama cha Wafanyabiashara wa Mitumba nchini humo (MCAK).
” … Katika miaka ya 1980, ungeweza kuona watu wakitembea bila nguo. Kwa sasa, hata watu wa kipato cha chini wanaweza kumudu mavazi,” anasema Lisa Kibutu, ambaye ni mbunifu wa mavazi nchini Kenya.
Ni kama anavyoeleza Najma Issa, mkazi wa jijini Dar es Salaam, akisema: “Nguo nyingi za mitumba zina ubora na zinadumu.” Maoni yake yanaungwa mkono na Juma Awadh, akiongeza: “Nanunua mitumba kwa sababu ya ubora na upekee wake.”
Tatu, soko la mitumba linahusisha ajira ya makundi mengi, kuanzia waagizaji, wauzaji wa jumla, mafundi wanaozifanyia ukarabati, na wauzaji wadogo, maarufu kwa jina la ‘wamachinga’.
Kwa upande mwingine, mnyororo huo unahusisha pia wafanyabiashara wa bidhaa zingine, zikiwamo chakula na vinywaji, walioko kwenye masoko ya mitumba katika miji ya Nairobi (Kenya), Kampala (Uganda) na Dar es Salaam (Tanzania).


