11 C
New York

Mafanikio sekta ya afya nchini 2021-26

Published:

Na Hassan Mwasha, Gazetini

KATIKA moja ya nukuu zake maarufu, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliwahi kutaja maradhi kuwa ni moja ya maadui watatu wa Taifa hili, akigusia pia umasikini na ujinga.

Kwa kulitambua hilo, Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, imeonesha nia ya dhati ya kuimarisha ubora na ufanisi wa mifumo ya utoaji wa huduma za afya hapa nchini.

Ni kama ilivyoelezwa na Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa hivi karibuni, Mei 11, 2026, wakati akiwasilisha Bajeti ya mwaka Mpya wa Fedha 2026/27 mbele ya Bunge la Bajeti la 13, Mkutano wa Tatu, kikao cha 26.

Katika hotuba yake, Waziri Mchengerwa alisema upatikanaji wa huduma umeongezeka kwa kasi, ambapo vituo vya afya vimeongezeka kutoka 10,153 mwaka 2021/2022 hadi 13,683 Machi 2026, likiwa ni ongezeko la vituo 3,530.

“Zahanati zimeongezeka kutoka 7,189 hadi 8,706, vituo vya afya 956 hadi 1,359, hospitali 404 hadi 475 na vituo vingine 1,604 hadi 3,143. Majengo mapya yameongezwa Muhimbili, KCMC, Mbeya, Benjamin Mkapa, Bugando, Mirembe, Kibongoto, Mtwara na Chato,” alisema.

Sambamba na hilo, alisema Serikali pia imejenga hospitali 10 mpya za rufaa za mikoa, kukarabati hospitali kongwe 50, kukamilisha maboma 980 ya zahanati, kujenga vituo vya afya 390, kuongeza mitambo ya oksijeni kutoka 25 hadi 61 na kujenga nyumba za watumishi zenye kuhudumia familia 540.

Kwa upande mwingine, alieleza namna Serikali kupitia Wizara ya Afya ilivyoimarisha huduma za dharura kwa kuongeza majengo ya EMD kutoka 7 hadi 125 kufikia Machi, 2026 na kuzifikisha kwa mara ya kwanza hadi ngazi ya afya ya msingi, ambako zaidi ya asilimia 80 ya Watanzania hupata huduma.

“Vitanda vya wagonjwa vimeongezeka kutoka 86,131 hadi 156,932, sawa na asilimia 82, na vitanda vya ICU katika vituo vya umma kutoka 258 hadi 1,647. Uwekezaji huu una maana ya kupokea wagonjwa kwa wakati, kupunguza msongamano na kuimarisha huduma kwa wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalum,” alisema Waziri Mchengerwa.

Wakati huo huo, Wizara ya Afya imefanikisha uimarishaji wa afya ya uzazi, mama na mtoto kwa kuongeza wodi za watoto wachanga kutoka 80 hadi 438, vituo vya upasuaji wa dharura kutoka 445 hadi 630, na vituo vya uchunguzi wa awali wa saratani ya mlango wa kizazi kutoka 732 hadi 1,700.

Kama hiyo haitoshi, upatikanaji wa dawa muhimu za afya ya uzazi, mama na mtoto umefikia asilimia 85. Akifafanua zaidi, Waziri Mchengerwa alisema:

“Mafanikio haya yamechangia kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi kutoka 556 kwa kila vizazi hai 100,000 mwaka 2016 hadi 104 mwaka 2022 na kuifanya Tanzania kutambuliwa barani Afrika kupitia uongozi wa Mheshimiwa Dk. Samia Suluhu Hassan.”

Wakati huo huo, Waziri Mchengerwa alieleza kuwa Serikali imedhamiria kupunguza zaidi vifo hivyo kwa asilimia 50 ifikapo mwaka 2030 na kuvuka lengo la dunia la chini ya vifo 70.

UBORA WA VIFAA, HUDUMA ZA KIBINGWA, DIPLOMASIA YA AFYA

Katika hotuba yake Bungeni mjini Dodoma, pia Waziri Mchengerwa aligusia uchunguzi, matibabu na huduma za ubingwa, akisema Serikali imenunua na kusimika vifaa vyenye thamani ya Shilingi bilioni 241.6.

“MRI zimeongezeka kutoka 7 hadi 13, CT Scan 12 hadi 45, Digital X-ray 147 hadi 559, Ultrasound 476 hadi 970, CathLab 1 hadi 4, Mini Angio Suite 5, Fluoroscopy 14 na PET CT Scan 1,” alisema.

Alisema sekta ya afya nchini imeshuhudia pia ongezeko kubwa la huduma za ubingwa na ubingwa bobezi, zikiwemo upandikizaji figo 170, uloto 57, vifaa vya usikivu 102, nyonga na magoti 3,037, na upasuaji wa mgongo 1,688.

Vilevile, kuna upasuaji wa ubongo kwa kufungua kichwa 1,208, kuzibua mishipa ya moyo 2,074, tiba ya mionzi ya ndani 10,056, immunotherapy 4,024 na uchunguzi wa saratani kwa PET-CT kwa wagonjwa 731.

Waziri Mchengerwa alibainisha kuwa ubora wa huduma, sambamba na ongezeko la vifaa umevutia wagonjwa 26,770 kutoka nchi jirani, hivyo kuimarisha tiba-utalii na diplomasia ya afya.

KUPANDA KIWANGO CHA CHANJO

Akiendelea kufafanua maendeleo makubwa yaliyopatikana katika sekta ya afya, Waziri Mchengerwa alisema watoto waliopata ‘Pentavalent’ dozi ya tatu wameongezeka kutoka 2,093,412 hadi 3,186,979, sawa na ongezeko la asilimia 52.2.

“Kiwango cha chanjo kimepanda kutoka asilimia 93 hadi 96, juu ya lengo la kimataifa la asilimia 90. Serikali imeratibu ununuzi wa dozi 161,499,930 za chanjo zenye thamani ya Sh bilioni 439.9, na hadi Machi 2026 kulikuwa na dozi 20,268,820 kwenye maghala,” alisema.

CHANGAMOTO UPATAKANAJI WA DAWA YADHIBITIWA

Waziri Mchengerwa alisema upatikanaji wa dawa na bidhaa za afya umeimarika baada ya Serikali kuoa Sh trilioni 1.4 kupitia MSD, ambapo Sh bilioni 150 zililipia madeni, bilioni 141.9 zilitumika kwa dawa za UKIMWI, malaria na kifua kikuu, na trilioni 1.1 kwa bidhaa za afya za vituo.

“Viwanda vipya 11 vya dawa na vifaa tiba vimeanzishwa, TPI Arusha kinafufuliwa ili kuzalisha dawa za VVU, na lita milioni 1.45 za viuadudu zenye thamani ya Shilingi bilioni 17.5 zimesambazwa katika halmashauri 184. Upatikanaji wa bidhaa muhimu 382 umeongezeka kutoka asilimia 58 mwaka 2021/2022 hadi asilimia 88 Machi 2026,” alisisitiza Waziri Mchengerwa.

AJIRA ZA KUTOSHA

Katika eneo la rasilimali watu, Serikali kupitia Wizara ya Afya imeajiri wataalamu 53,633 kuanzia mwaka 2021 hadi Machi 2026 na kufanya watumishi wake kufikia 182,430. Watumishi 9,039 wameajiriwa kwa mikataba ya muda mfupi kupitia mapato ya ndani.

Kama hiyo haitoshi, kupitia ‘Samia Health Super Specialization Scholarship Program’, wataalamu 2,982 wamepata mafunzo ya ubingwa na ubingwa bobezi, ikilinganishwa na 961 katika kipindi cha 2016/2017 hadi 2020/2021.

BIMA YA AFYA KWA WOTE

Akizungumzia hilo, Waziri Mchengerwa alisema Bima ya Afya kwa Wote nayo imeanza baada ya sheria kupitishwa Novemba 2023, ambapo hadi Machi, 2026, Serikali imetoa Shilingi bilioni 48.8, kaya 172,297 zimefikiwa na wananchi 463,228 wamesajiliwa.

“Mheshimiwa Spika, mafanikio haya si takwimu tu za majengo, vitanda, vifaa na huduma; ni simulizi ya maisha yaliyookolewa, matumaini yaliyorejeshwa na utu wa Mtanzania uliolindwa.

“Kama ambavyo Mwalimu Nyerere aliamini kuwa maendeleo ya kweli ni maendeleo ya watu, na kama Nelson Mandela alivyotufundisha kuwa heshima ya binadamu ndiyo msingi wa taifa huru.

“Kila zahanati iliyojengwa, kila hospitali iliyoboreshwa, kila mama aliyepata huduma salama na kila mgonjwa aliyepata huduma karibu na nyumbani ni ushahidi kuwa Tanzania inaendelea kujenga taifa lenye afya, usawa, utu na matumaini,” alisema.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img