9.5 C
New York

Siku ya Usalama kazini 2026: Mambo muhimu kujua

Published:

Na mwandishi wetu, Gazetini

SERIKALI imesema jumla ya watu 3,557 wamepata ajali wakiwa kazini katika kipindi cha miaka mitatu kuanzia 2023 hadi 2025, huku watu 169 wakipoteza maisha kutokana na matukio hayo, hali inayoonesha ukubwa wa changamoto ya usalama na afya mahala pa kazi nchini.

Takwimu hizo zimetolewa wakati Tanzania ikijiandaa kuungana na mataifa mengine duniani kuadhimisha Siku ya Usalama na Afya Mahala pa Kazi, ambayo huadhimishwa kila mwaka Aprili 28 na mwaka huu kitaifa itafanyika mkoani Njombe.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Wakala wa Usalama na Afya Mahala pa Kazi (OSHA), ikimnukuu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Mahusiano Kazini), Deus Sangu, ajali na vifo vinavyotokea mahala pa kazi vinaendelea kuwa tishio kwa ustawi wa wafanyakazi na maendeleo ya uchumi wa taifa.

Amesema vifo hivyo vinaathiri si tu familia za waathirika bali pia uzalishaji na nguvu kazi ya taifa, akisisitiza umuhimu wa kuimarisha mifumo ya kinga na usimamizi wa sheria za usalama kazini.

“Serikali itaendelea kusimamia utekelezaji wa sheria ya usalama na afya mahala pa kazi ili kuhakikisha maeneo yote ya kazi yanakuwa salama na yenye mazingira rafiki kwa wafanyakazi,” amesema Waziri Sangu.

Ameeleza kuwa Serikali kupitia OSHA imeendelea kuimarisha utekelezaji wa sera na sheria mbalimbali zinazolenga kuwalinda wafanyakazi dhidi ya ajali, magonjwa ya kazini na vifo vinavyotokana na mazingira hatarishi ya kazi.

Katika ngazi ya dunia, Shirika la Kazi Duniani (ILO) linaonesha kuwa zaidi ya watu milioni 2.93 hufariki kila mwaka kutokana na sababu zinazohusiana na kazi zao, huku watu milioni 395 wakipata majeraha makubwa kazini.

Aidha, shirika hilo limebainisha kuwa wafanyakazi bilioni 2.41 huathiriwa na joto kali kila mwaka, hali inayoongeza hatari ya magonjwa, uchovu kupita kiasi na kupungua kwa tija kazini.

Kwa mujibu wa ILO, zaidi ya watu 840,000 pia hufariki kila mwaka kutokana na matatizo ya kiafya yanayotokana na hatari za kisaikolojia mahala pa kazi, ikiwamo kufanya kazi kwa muda mrefu, kukosa uhakika wa ajira na unyanyasaji kazini.

Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda akizungumza jambo wakati wa kikao cha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Mahusiano), Deus Sangu akizungumza na waandishi wa habari, Aprili 23, 2026 Jijini Dar es Salaam wakati akitoa taarifa kuhusu maadhimisho ya Siku ya Usalama na Afya Mahala pa Kazi Duniani ambayo yanatarajiwa kufanyika Aprili 28, 2026 mkoani Njombe

Hatari hizo zimehusishwa moja kwa moja na ongezeko la magonjwa ya moyo, matatizo ya afya ya akili, msongo wa mawazo na hata visa vya kujiua.

Kwa mujibu wa Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda, maandalizi ya maadhimisho hayo yamekamilika na taasisi hiyo imejipanga kuhakikisha tukio hilo linakuwa jukwaa la kuongeza uelewa kuhusu umuhimu wa usalama na afya katika maeneo ya kazi nchini.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img