21.4 C
New York

Ebola katikati ya Serikali, waasi wa M23

Published:

KINSHASA, DRC

KUNDI la waasi la M23 linajivunia idadi ndogo ya maambukizi ya Ebola katika maeneo yake, likidai kuwa hilo linathibitisha uwezo wake mkubwa wa kuongoza.

M23 wanashikilia maeneo mengi ya Kaskazini na Kusini mwa majimbo ya Kivu, pia operesheni yao ya mwaka 2025 ikiwapatia miji mikubwa miwili ya Mashariki, Goma na Bukavu.

Madai ya Umoja wa Mataifa na jumuhiya zingine za kimataifa ni kwamba Kundi hilo linaungwa mkono na Serikali ya Rwanda.

Kwa mujibu wa ripoti ya Wizara ya Afya ya DRC na ile ya Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa (WHO), maeneo yaliyo chini ya waasi yalikuwa na watu wanne pekee waliopata maambukizi ya Ebola.

Juni, 2026, M23 iliibuka na taarifa kuwa tayari imetokomeza Ebola baada ya siku 21 za upimaji katika maeneo yake.

Freddy Kaniki, Mratibu wa Afya wa M23, alisema mafanikio hayo yametokana na mikakti mizuri ya uongozi wa Kundi hilo katika kukabiliana na ugonjwa huo.

Miongoni mwa mikakati iliyotumika ni kuwatenga wenye maambukizi, pia kutangaza karantini ya siku 15 kwa kila msafiri aliyetokea maeneo yaliyo chini ya Serikali.

Wakati hali ikiwa hivyo huko kwa waasi, kiwango cha maambukizi ya Ebola kimeripotiwa kuwa cha juu katika maeneo mengine yaliyo chini ya Serikali.

Ripoti ya hivi karibuni ya Serikali inaonesha kuwa maambukizi yamefikia 1,873 na watu zaidi ya 600 wamepoteza maisha.

“M23 inataka kuonesha kwa vitendo kuwa inaweza kufanya kazi kama dola kwa kusimamia vizuri afya ya umma kuliko Serikali ya DRC,” anasema Reagan Miviri, mchambuzi kutoka Taasisi ya Ebuteli mjini Kinshasa.

Lakini, bado mafanikio hayo ya M23 yanahusishwa na msaada kutoka kwa ni jirani ya Rwanda, ikitajwa kuwezesha dawa, vifaa na hata wataalamu wa afya.

Taarifa ambazo Rwanda imeendelea kukanusha zinadai kuwa ilishaipa M23 msaada wa dawa na vifaa wenye thamani ya Dola 6,891 kufikia Juni 18, 2026.

Related articles

Recent articles