22.9 C
New York

Suruali ya jinzi ingekwamisha usajili staa Chelsea

Published:

LONDON, Uingereza

MIONGONI mwa nyota wapya waliotua Chelsea majira haya ya kiangazi ni Geovany Quenda, ambaye amekiri kuwa ni shabiki mkubwa wa Cristiano Ronaldo.

Quenda alizaliwa barani Afrika katika nchi ya Guinea-Bissau lakini familia yake ilihamia Ureno akiwa na umri wa miaka saba.

Ametua Stamford Bridge akitokea katika ‘academy’ ya Sporting Lisbon na wachambuzi wengi wanafananisha uchezaji wake na ule wa winga wa Arsenal, Bukayo Saka.

Hata hivyo, katika maisha yake ya kutafuta njia ya ‘kutoka’, Quenda aliwahi kuzuiwa kufanya majaribio katika academy ya klabu ya Damaiense ya huko Ureno.

Siku hiyo, alifika mapema na wazazi wake kwa ajili ya majaribio lakini kuvaa jinzi kulisababisha awekwe kando wakati wenzake wanaanza kucheza.

Akiwa nje, mpira uliotoka na kumfikia mguuni ulibadili stori. Kwa namna alivyoutuliza na kukokota, kocha Ana Correia akavutiwa na uwezo wake na kuwashawishi mabosi wampe nafasi.

Baada ya kucheza U-10 ya Damaiense, klabu kubwa ya Ureno, Benfica, ilimchukua, kabla ya wapinzani wao wakubwa, Sporting, kumsajili.

Akiwa na umri wa miaka 16, Quenda alishaanza kufanya mazoezi na timu ya wakubwa ya Sporting, wakati huo kocha akiwa Ruben Amorim.

Ilimchukua dakika 24 tu kufunga bao katika mechi yake ya kwanza (dhidi ya Porto). Rekodi iliyofuata ni kuwa mchezaji mdogo zaidi kuifungia Sporting katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Ni rekodi ambayo awali ilikuwa ikishikiliwa na Ronaldo alipokuwa na Sporting miaka mingi iliyopita.

Kama hiyo haitoshi, ‘dogo’ akawa mchezaji mwenye umri mdogo kufunga bao katika historia ya Ligi Kuu ya Ureno.

Mkataba aliosaini Chelsea utafikia ukomo mwaka 2034. Katika safari yake ya jijini London, Quenda aliongozana na baba, mama, dada, marafiki na wakala wake, Basaula Lemba.

Lemba ni mkongwe wa Ligi Kuu ya Ureno, pia akicheza mechi 10 za timu ya soka ya Taifa ya Zaire (sasa DRC).

Related articles

Recent articles