26.5 C
New York

Mjadala mzito timu 64 kushiriki Kombe la Dunia

Published:

NYON, Uswis

MOJA ya alama za uongozi wa Gianni Infantino katika miaka yake 10 ndani ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) ni kuongeza timu shiriki kwenye fainali za Kombe la Dunia, kutoka 32 hadi 48.

Kuelekea fainali zijazo za mwaka 2030 zitakaofanyika Hispania, Ureno na Morocco, Infantino anapigania wazo lake jingine – kuongeza idadi na kufikia timu 64.

Hoja yake ni ile ile, kwamba ongezeko la timu linazipa nchi changa nafasi ya kuingia kwenye mashindano hayo makubwa zaidi katika ulimwengu wa soka.

“Kama hatuyapi mataifa madogo nafasi ya kushiriki, hayatoweza kukua na kuimarika,” amesema Rais huyo.

Katika hilo, Infantino anaungwa mkono na Rais wa Shirikisho la Soka la Amerika ya Kusini (CONMEBOL), Alejandro Dominguez.

Katika hilo, wanatolea mfano ongezeko la timu msimu huu lilivyozipatia nchi kama Cape Verde na Caracao nafasi ya kuionesha dunia uwezo wake kupitia michuano ya Kombe la Dunia.

Hata hivyo, Rais wa Shirikisho la Soka la Ulaya (UEFA), Aleksander Ceferin, hakubaliani na wazo hilo, akisema itapunguza upekee na ushindani wa mashindano hayo.

Ni kama anavyoamini Rais wa Shirikisho la Soka la Amerika ya Kati na Caribbean (CONCACAF), Victor Montagliani, akidai kuwa ongezeko la timu linapunguza ushindi wa michuano hiyo.

Kwa upande wake, Rais wa Shirikisho la Soka barani Asia (AFC), Sheikh Salman bin Ibrahim Al Khalifa, ameita kuwa ni fujo kwa Kombe la Dunia kushirikisha timu nyingi.

Kwa pamoja, viongozi hao wanajenga hoja kuwa timu yenye uwezo mzuri uwanjani inaweza kufuzu pasi na kutegemea idadi kuongezeka.

Je, ni kweli ongezeko la timu 64 lina tija kama anavyodai Infantino au UEFA, CONCACAF na AFC wako sahihi kwamba inashusha hadhi ya michuano ya Kombe la Dunia?

Related articles

Recent articles