26.5 C
New York

Hispania ilivyojenga utawala wake soka la Ulaya

Published:

LONDON, Uingereza

MIAKA 16 tangu ilipotwaa Kombe la Dunia, timu ya soka ya Taifa ya Hispania imerudisha ufalme wake baada ya kuwa mabingwa wa msimu huu.

Mara ya mwisho kwa La Roja kuwa mabingwa wa michuano hiyo ilikuwa mwaka 2010 nchini Afrika Kusini.

Safari hii, wamebeba ‘ndoo’ kwa kuifunga Argentina bao 1-0 katika mchezo wa fainali uliochezwa juzi Julai 19, 2026 kwenye Uwanja wa MetLife, New Jersey, Marekani.

TUZO KAMA ZOTE

Katika fainali za mwaka huu, tuzo ya Mchezaji Bora imetua kwa kiungo wao anayekipiga Manchester City, Rodri.

Hiyo inakuwa tuzo kubwa ya tatu katika maisha ya soka ya nyota huyo mwenye umri wa miaka 30 baada ya Ballon d’Or (2023) na Mchezaji Bora wa Euro (2024).

Pia, tuzo ya Kipa Bora msimu huu wa Kombe la Dunia imetua Hispania, akiichukua Unai Simon, ambaye aliruhusu bao moja tu katika mechi nane, saba akicheza bila kuruhusu nyavu zake kutikiswa.

Mchezo pekee alioruhusu bao ni ule waliokutana na Ubelgiji katika robo fainali, hiyo ikithibitisha kuwa kocha Luis de la Fuente hakukosea kumuamini mbele ya kipa wa Arsenal, David Raya.

Tuzo ya Kinda Bora pia imetua Hispania, kwa beki wa kati mwenye umri wa miaka 19, Pau Cubarsi, ambaye aliifanya Argentina kupiga mashuti mawili pekee siku ya fainali.

KABATI LIMEJAA MAKOMBE

Ni miaka miwili tu tangu Hispania ilipotwaa taji la EURO 2024, kama walivyofanya mwaka 2010, ambapo pia walitoka kuwa mabingwa wa EURO 2008.

Hispania inakuwa nchi ya kwanza kutwaa mataji mawili ya Kombe la Dunia kwa wakati mmoja, baada ya timu yao ya wanawake kuwa mabingwa wa mashindano hayo mwaka 2023.

Timu yao ya wanawake pia ndiyo washindi wa Ligi ya Mataifa ya Ulaya (UEFA Nations League) kwa miaka miwili mfululizo (2024 na 2025).

Pia, kama itakumbukwa, timu ya wanaume ni mabingwa wa Nations League mwaka 2023 na michuano ya Olimpiki mwaka 2024.

Kuanzia vijana wao wa kike na wa kiume wa U-17, U-19, U-20 na U-21, pamoja na timu za wakubwa, Taifa la Hispania limekusanya mataji makubwa 16 ndani ya miaka mitano ya hivi karibuni.

SIRI YA MAFANIKIO

Shirikisho la Soka la Hispania lilipomtangaza Luis de la Fuente kuwa kocha wa La Roja, wengi hawakutatajia kuona kocha huyo akitwaa Nations League (2023), EURO (2024) na Kombe la Dunia (2026) ndani ya muda mfupi.

Alipewa kazi baada ya Hispania ya Luis Enrique kuishia hatua ya 16 Bora katika fainali za mwaka 2022, ambapo waliondoshwa na Morocco iliyofika nusu fainali.

De La Fuente alipewa ajira akiwa hana ‘CV’ ya kufanya kazi katika klabu kubwa yoyote. Kwa wachambuzi wengi, Shirikisho la Soka la Hispania lilicheza kamari kwa kocha huyo.

Hata hivyo, alikuwa na silaha kubwa moja. Aliwahi kufanya kazi na wachezaji wengi wa kikosi hicho akiwa kocha wao wa timu za vijana za U-19 na U-21.

“De la Fuente alikuwa anawafahamu wachezaji wengi wa Hispania kwa kuwa alikuwa nao kwenye timu za vijana,” anasema staa wa zamani wa timu hiyo, Juan Mata.

Kwa sasa, Hispania haijafungwa katika mechi zote 38 ilizocheza hivi karibuni. Hakuna timu ya taifa barani Ulaya au Amerika Kusini yenye mwenendo mzuri kiasi hicho.

MOTO UNAENDELEA

Kesho ya timu ya soka ya Taifa ya Hispania inawapa matarajio makubwa mashabiki wake. Lamine Yamal na beki Pau Cubarsi wamebeba Kombe la Dunia wakiwa na umri wa miaka 19 tu kila mmoja.

Yamal ameandika historia ya kuwa mchezaji mwenye umri mdogo zaidi kucheza fainali baada ya Pele (1958) na Giuseppe Bergomi (1982).

Katika soka la wanawake, pia Hispania ina matarajio makubwa kwa Vicky Lopez, ambaye licha ya umri wake wa miaka 19, tayari ana mataji matatu ya Ligi ya Mabingwa Ulaya akiwa na Barcelona.

Mshambuliaji Salma Paralluelo hajafikisha miaka 23 lakini tayari ana mechi zaidi ya 50 akiwa na ‘uzi’ wa timu ya taifa.

“Nipongeze mfumo unaotumika. Kwa sababu Hispania hajawahi kuwa hivi. Naamini wana miaka mingi ya kutawala,” amesema lejendari wa Arsenal na timu ya soka ya Taifa ya Ufaransa, Thierry Henry.

Related articles

Recent articles