LONDON, Uingereza
MAPEMA wiki hii, klabu ya Chelsea ilitumia kitita cha Pauni milioni 117 kuinasa saini ya mshambuliaji wa kimataifa England kutoka Aston Villa, Morgan Rogers.
Ukame wa mabao ni moja ya shida zilizoisumbua Chelsea msimu uliopita na Rogers alifunga mara 14 na kutoa ‘asisti’ 12 katika mechi 55 za msimu uliopita (2025-26).
Nyota huyo amesaini mkataba wa miaka sita wenye kipengele cha kuongezewa mwaka mmoja endapo atafanya vizuri Stamford Bridge.
MSAKO WA MIAKA MIWILI
Blues wamekuwa wakiifuatilia saini ya Rogers kwa miaka miwili na hivi karibuni alihusishwa zaidi na majirani zao wa London, Arsenal.
Ukiacha kazi kubwa iliyofanywa na Xabi Alonso na tajiri Behdad Eghbali, nyota hao wa Chelsea anaocheza nao England, Reece James na Cole Palmer, nao wametajwa kumshawishi kujiunga na klabu hiyo.
Mwaka 2024, Chelsea walikaribia kumsajili Rogers, ambako walikuwa tayari kuipa Villa kiasi cha fedha, pamoja na straika Nicolas Jackson.
ATAINGIAJE KIKOSINI?
Ni wazi kocha Xabi Alonso atatumia mfumo wa mabeki wa kati watatu, ambao ulimpa taji la Bundesliga akiwa na kikosi cha Bayern Leverkusen.
Moja ya vyanzo vya habari kinaeleza kuwa kuna uwezekano mkubwa wa Rogers kucheza winga ya kushoto, ambako pia yupo Jamie Gittens.
Palmer atacheza kiungo mshambuliaji (namba 10), huku Estevao Willian, Pedro Neto na Geovany Quenda wakigombea nafasi kwenye eneo la winga ya kulia.
Tayari eneo la mshambuliaji wa kati (namba 9) lina Joao Pedro, Nicolas Jackson, Liam Delap, Emmanuel Emegha na Marc Guiu.
CHELSEA HAWATANII
Kabla ya Rodgers, tayari Blues wakitumia Pauni milioni 47 kuinasa saini ya beki wa pembeni kutoka Atalanta ya Italia, Marco Palestra.
Pia, tayari Blues imewanasa mabeki wengine wawili, Pep Chavarria kutoka Rayo Vallecano na Maxence Lacroix aliyekuwa Crystal Palace.
Wakati huo huo, klabu hiyo ya Magharibi mwa Jiji la London imeshamalizana na ‘fundi’ wa eneo la kiungo kutoka katika kikosi cha Strasbourg ya Ufaransa,
Valentin Barco.
Aidha, Chelsea imevuna zaidi ya Pauni milioni 120 kwa kuwauza Marc Cucurella (Real Madrid), Andrey Santos (Manchester United), Tyrique George (Everton), na Jimmy-Jay Morgan (West Brom).


