PARIS, Ufaransa
KOCHA wa zamani wa Real Madrid, Zinedine Zidane, amesaini mkataba wa kuliongoza benchi la ufundi la timu ya soka ya Taifa ya Ufaransa.
Zidane anatua kwenye benchi kuchukua nafasi ya Didier Deschamps aliyeachia ngazi baada ya fainali za Kombe la Dunia za mwaka huu.
Deschamps alisimamia mechi yake ya mwisho wakati Ufaransa ilipotandikwa mabao 6-4 na England katika mchezo wa kusaka mshindi wa tatu kwenye mashindano hayo.
Kwa upande wake, ‘Zizou’ alishafanya mazungumzo na kukubaliana na mabosi wa Shirikisho la Soka la Ufaransa (FFF) tangu Novemba, 2025.
Katika taarifa yake kupitia mtandao wa kijamii wa X, mwandishi wa habari maarufu wa Italia, Fabrizio Romano, amesema Zidane amesaini mkataba wa muda mrefu.


