8 C
New York

Céline Dion kurejea jukwaani baada ya miaka minne

Published:

Na Mwandishi Wetu, Gazetini

MWIMBAJI maarufu duniani, Céline Dion, ametangaza rasmi kurejea jukwaani, miaka minne baada ya kugundulika kuwa na ugonjwa sugu uliomuathiri sauti yake ya uimbaji pamoja na uwezo wa kutembea.

Dion, anayefahamika kwa nyimbo maarufu kama My Heart Will Go On na Because You Loved Me, anatarajiwa kufanya maonyesho ya mfululizo wa siku 10 katika ukumbi wa Paris La Défense Arena wenye uwezo wa kubeba watu 40,000, yatakayofanyika kati ya Septemba na Oktoba mwaka huu.

Tangazo hilo limetolewa siku ya kuzaliwa kwake ya miaka 58, ambapo kupitia ukurasa wake wa Instagram, Dion amesema kurejea kwake jukwaani ni “zawadi bora zaidi katika maisha yake.”

“Niko tayari sana kufanya hili. Najisikia vizuri, nina nguvu na nina hamasa, japokuwa pia nina wasiwasi kidogo,” amesema.

Akizungumzia hali yake ya afya, Dion amesema anaendelea vizuri na ameanza kurejea katika shughuli za muziki.

“Ninaendelea vizuri, ninasimamia afya yangu na najisikia vizuri. Nimeanza kuimba tena, hata kufanya mazoezi kidogo ya kucheza,” alisema, akiwashukuru mashabiki wake kwa sala, upendo na msaada waliompa katika kipindi kigumu.

Tiketi zatarajiwa kuwania kwa wingi

Dion, ambaye ni miongoni mwa wasanii waliouza rekodi nyingi zaidi duniani, hajafanya tamasha lake binafsi tangu Machi 8, 2020, huko Newark, New Jersey. Ziara yake ya Courage ilisimamishwa kutokana na janga la Covid-19, kabla ya kugundulika kuwa na ugonjwa wa Stiff Person Syndrome (SPS) uliomlazimu kufuta maonyesho yote yaliyosalia.

Kwa kurejea kwake, tarehe za matamasha zimepangwa kwa vipindi ili kupunguza uchovu wa mwili. Tiketi zitaanza kuuzwa Aprili 7, huku mashabiki wakiruhusiwa kujiandikisha mapema kuanzia Machi 31.

Tangazo la kurejea kwake lilipokelewa kwa shangwe jijini Paris, ambapo Mnara wa Eiffel uliwashwa taa zenye ujumbe “Paris, niko tayari,” na nyimbo zake maarufu kupigwa kuashiria ujio wake.

Mapambano na ugonjwa

Dion alitangaza Desemba 2022 kuwa anaugua ugonjwa wa Stiff Person Syndrome, unaoathiri mfumo wa neva na kusababisha misuli kukaza na kuathiri uwezo wa kutembea na kuimba. Ugonjwa huo hauna tiba kamili.

Akizungumza awali, alisema hali hiyo iliathiri sana maisha yake ya kila siku, ikiwemo sauti yake.

“Ni kama mtu anakukaba koo,” aliwahi kueleza.

Hata hivyo, Dion amesisitiza kuwa hakukata tamaa. Ameeleza kuwa amekuwa akifanya mazoezi makali ya kimwili na ya sauti mara tano kwa wiki kwa kushirikiana na madaktari.

Juhudi hizo zilianza kuzaa matunda mwaka 2024, aliporejea jukwaani kwa hisia kali katika ufunguzi wa Michezo ya Olimpiki ya Paris, akiimba wimbo wa Edith Piaf Hymne à l’Amour kutoka Mnara wa Eiffel.

Kurejea kwake sasa kunatarajiwa kuwa moja ya matukio makubwa ya muziki duniani mwaka huu, huku mashabiki wakisubiri kwa hamu kumuona tena jukwaani baada ya safari yake ndefu ya mapambano na ugonjwa.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img