5.5 C
New York

Dk. Yonazi ateta na bosi mpya TACAIDS, Tanzania yaendelea kudhibiti UKWIMWI

Published:

Na mwandishi wetu, Gazetini

Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu, Dk. Jim Yonazi, amekutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi Mtendaji mpya wa Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS), Dk. Adam Mrisho, aliyefika kujitambulisha kufuatia uteuzi wake uliofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan.

Kikao hicho kimefanyika leo Machi 23, 2026 katika Ofisi ya Waziri Mkuu, mtaa wa Reli jijini Dodoma, kikihudhuriwa pia na Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi hiyo, Dk. James Kilabuko, pamoja na Mratibu wa Masuala ya UKIMWI, Adela Mpina.

Katika mazungumzo hayo, Dk. Yonazi amempongeza Dk. Mrisho kwa kuaminiwa kushika nafasi hiyo, akisisitiza umuhimu wa kuimarisha uratibu wa mapambano dhidi ya UKIMWI nchini. Alimhakikishia ushirikiano wa karibu kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu ili kuhakikisha utekelezaji wa majukumu ya TACAIDS unaendelea kwa ufanisi.

Mazungumzo hayo yamekuja wakati ambapo Tanzania inaendelea kurekodi mafanikio makubwa katika mwitikio dhidi ya UKIMWI chini ya uongozi wa Rais Samia. Kwa mujibu wa taarifa ya TACAIDS, kiwango cha watu wanaotambua hali zao za maambukizi ya VVU kimeongezeka kutoka asilimia 91 mwaka 2024 hadi asilimia 92 mwaka 2025.

Aidha, idadi ya watu wanaoishi na virusi vya UKIMWI (WAVIU) wanaotumia dawa za kufubaza VVU (ARV) imeongezeka kutoka asilimia 98 hadi asilimia 98.5, huku asilimia ya waliofanikiwa kufubaza virusi hivyo ikipanda kutoka 97 hadi 98.1 katika kipindi hicho. Mafanikio hayo yanaenda sambamba na upanuzi wa huduma, ambapo vituo vinavyotoa tiba na matunzo kwa WAVIU vimeongezeka kutoka 7,805 mwaka 2024 hadi kufikia 8,203 mwaka 2025.

Takwimu hizo zinaonyesha pia kupungua kwa kasi ya maambukizi mapya ya VVU, kutoka zaidi ya watu 150,000 kwa mwaka mwanzoni mwa miaka ya 1990 hadi kufikia watu 43,000 mwaka 2025. Vilevile, vifo vinavyotokana na UKIMWI vimepungua kwa kiasi kikubwa kutoka zaidi ya watu 100,000 mwaka 2000 hadi kufikia watu 24,000 mwaka 2025.

Katika kuhakikisha mafanikio hayo yanaendelezwa, Serikali kupitia Mfuko wa Udhamini wa Kudhibiti UKIMWI (ATF) inapanga kukusanya zaidi ya shilingi bilioni 277 kutoka vyanzo vya ndani ili kugharamia huduma za VVU na UKIMWI nchini.

Sambamba na hilo, juhudi zinaendelea kuimarishwa katika huduma za kinga, hasa kwa makundi yaliyo katika hatari zaidi, yakiwemo vijana wa miaka 15 hadi 24, wachimbaji wadogo wa madini, wavuvi, madereva wa masafa marefu, wanawake wanaofanya biashara ya ngono pamoja na watu wanaotumia dawa za kulevya kwa njia ya kujidunga.

Elimu kwa umma imeendelea kutajwa kuwa nguzo muhimu katika mapambano hayo, hasa katika kupunguza unyanyapaa unaoweza kuzuia wananchi kupata huduma stahiki. Serikali inaamini kuwa kwa kuendelea kuwekeza katika kinga, tiba na elimu, inawezekana kudhibiti na hatimaye kutokomeza UKIMWI nchini.

Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu, Dk. Jim Yonazi(kushoto), akiwa kwenye picha ya pamoja na Mkurugenzi Mtendaji mpya wa Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS), Dk. Adam Mrisho.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img