18.5 C
New York

Ummy awahimiza watumishi kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa bajeti ya Serikali

Published:

Na mwandishi wetu, Gazetini

NAIBU Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), Ummy Nderiananga, amewahimiza watumishi wa ofisi hiyo kuongeza bidii, ufanisi na weledi katika utendaji wao ili kuhakikisha malengo yaliyowekwa katika bajeti ya Serikali yanatekelezwa kwa ufanisi.

Akizungumza juzi jijini Dodoma wakati wa ufunguzi wa Baraza la Wafanyakazi, Ummy aliyemwakilisha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), William Lukuvi-alisisitiza umuhimu wa ushirikiano na uwajibikaji miongoni mwa watumishi katika kutekeleza majukumu yao ya kila siku.

Alieleza kuwa mabaraza ya wafanyakazi yameanzishwa kufuatia Tamko Na. 1 la mwaka 1970 lililotolewa na Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, likilenga kuimarisha ufanisi na tija katika maeneo ya kazi.

“Kupitia mabaraza haya, wafanyakazi na waajiri hupata jukwaa la kujadili masuala mbalimbali na kubadilishana mawazo kwa manufaa ya taasisi. Ni matarajio yangu kuwa majadiliano yenu yatajikita katika kuboresha utendaji wa Ofisi ya Waziri Mkuu,” alisema Ummy.

Awali, Katibu Mkuu wa Ofisi hiyo, Dk. Jim Yonazi, alimshukuru Waziri wa Nchi pamoja na Naibu Waziri kwa kushiriki katika kikao hicho muhimu cha Baraza la Wafanyakazi.

Aidha, aliwapongeza viongozi hao kwa ushindi walioupata katika Uchaguzi Mkuu na kwa kuendelea kuaminiwa na Rais kuongoza na kusimamia sekta hiyo nyeti.

Dk. Yonazi alibainisha kuwa kikao hicho kimewakutanisha Menejimenti ya Ofisi ya Waziri Mkuu pamoja na wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi kwa lengo la kujadili na kupitia rasimu ya bajeti ya ofisi hiyo, ikiwemo tathmini ya utekelezaji wake, kabla ya kuidhinishwa na kuwasilishwa katika ngazi zinazofuata.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img