TEHRAN, Iran
VITA vinavyoendelea kati ya Marekani na Israel zilizoungana kuishambulia Iran vinatajwa kuathiri sekta ya utalii Mashariki mwa Kati.
Kwa mujibu wa Shirika la Utalii la Umoja wa Mataifa (UNWTO), sekta ya utalii ilishapiga hatua kubwa katika nchi za Mashariki ya Kati na Afrika ya Kaskazini.
“Kwa mwaka 2025 pekee, watalii wa kimataifa takribani milioni 100 walitembelea nchi kama Misri na Jordan, kama ilivyo kwa Qatar na Saudi Arabia,” inaeleza ripoti ya UNWTO.
“Kiwango hicho ni ongezeko la asilimia 39, ukilinganisha na takwimu za mwaka 2019, kabla ya janga la Corona kutangazwa.”
Kwa takwimu hizo, hakuna eneo jingine duniani lililoizidi Mashariki ya Kati na Afrika ya Kaskazini kwa kasi ya maendeleo ya sekta ya utalii.
Hata hivyo, vita vinavyoendelea, ambapo vikosi vya kijeshi vya Marekani na Israel vinashambuliana na Iran, sekta ya utalii inatarajiwa kutikiswa.
Kwa sasa, shughuli za utalii zinapitia nyakati ngumu si tu kwa sababu ya watalii kuhofia kwenda, bali pia kutokana na kufungwa kwa anga katika baadhi ya nchi za Mashariki ya Kati.
Hilo linajidhihirisha wazi katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Dubai, Mji Mkuu wa Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE).
Kwa mwaka 2025, ndiyo uwanja wa ndege pekee duniani uliohudumia wasafiri wengi, zaidi ya watu milioni 95.
Katika mazingira ya sasa ya vita, haitegemewi kuona uwanja huo ukiendelea kufanya biashara kwa kiwango hicho.
Kuyumba kwa sekta ya utalii kunatarajiwa kuzikumba pia Qatar, Saudi Arabia, Misri, Tunisia, Jordan na Morocco, ambazo zimewekeza mabilioni ya fedha katika utalii.
Katika Dira ya Mwaka 2030, Saudi Arabia imewekeza fedha nyingi ikitarajia kupokea watalii milioni 70 kwa mwaka.


