Na mwandishi wetu, Gazetini
Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati anayeshughulikia Mafuta na Gesi, Dk. James Mataragio, ameielekeza Mamlaka ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) kuongeza kasi ya utafiti wa awali katika maeneo mapya yenye mafuta na gesi asilia ili kuvutia wawekezaji zaidi na kuongeza mapato ya taifa.
Dk. Mataragio ametoa maelekezo hayo Februari 26, 2026, wakati akizungumza katika Mkutano wa Tano wa Baraza la Wafanyakazi wa PURA uliofanyika mkoani Morogoro, ambapo alisisitiza kuwa juhudi hizo ni muhimu katika kuchochea uwekezaji, kupanua ushiriki wa wazawa na kuimarisha utekelezaji wa majukumu ya msingi ya mamlaka hiyo.

Amesema ni wajibu wa PURA kuendelea kubaini na kuendeleza maeneo mapya yenye fursa za miradi ya mafuta na gesi, kuyatangaza kwa wawekezaji pamoja na kuhakikisha usimamizi madhubuti wa shughuli zote zilizo chini ya mamlaka yake kulingana na malengo ya kuanzishwa kwake.
Amefafanua kuwa majukumu ya PURA yanajumuisha kusimamia na kufuatilia shughuli za utafutaji na uzalishaji wa mafuta na gesi asilia kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zilizopo, kuishauri Serikali kuhusu masuala ya mkondo wa juu wa sekta hiyo, pamoja na kutangaza vitalu vilivyowazi kwa ajili ya uwekezaji ili kuongeza ugunduzi wa rasilimali nchini.
Kwa mujibu wa Dk. Mataragio, utekelezaji wa hatua hizo utaongeza mchango wa sekta ya mafuta na gesi katika kukuza uchumi wa taifa, kuimarisha usimamizi wa rasilimali za asili na kuhakikisha Watanzania wananufaika zaidi na rasilimali hizo.


