-Kuchochea uchumi wa buluu
Na mwandishi wetu, Gazetini
SERIKALI imezindua mpango mahsusi wa kusambaza mifumo ya umeme jua katika visiwa 120 nchini, hatua inayolenga kuchochea Uchumi wa Buluu na kuharakisha upatikanaji wa nishati safi kwa wananchi wa maeneo ya pembezoni.
Kupitia mpango huo, jumla ya mifumo 20,000 ya umeme jua itafungwa kwa gharama ya Shilingi bilioni 8, huku Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, akiweka ruzuku ya hadi asilimia 75 ya gharama za uunganishaji umeme ili kupunguza mzigo kwa wananchi.
Akizindua mradi huo Leo Februari 21, 2026 katika Kisiwa cha Bezi, wilayani Ilemela mkoani Mwanza, Naibu Waziri wa Nishati, Salome Makamba, amesema maeneo ya visiwani na delta yana changamoto za kipekee zikiwemo umbali kutoka Gridi ya Taifa, gharama kubwa za usafirishaji wa vifaa na mtawanyiko wa makazi.
“Hata hivyo, changamoto hizi haziwanyimi wananchi haki ya kupata huduma ya umeme. Serikali imekuja na suluhisho la mifumo ya umeme jua pamoja na gridi ndogo ili kuwafikia wananchi kwa haraka,” amesema.
Mradi huo unatekelezwa chini ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA) na unatarajiwa kuimarisha shughuli za kiuchumi ikiwemo uvuvi, ufugaji wa samaki, kilimo cha mwani na utalii wa fukwe na visiwa.

Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati (Umeme na Nishati Jadidifu), Mhandisi Edson Ngabo, amesema wananchi wanapaswa kutumia umeme huo kuongeza thamani ya mazao na bidhaa zao badala ya matumizi ya nyumbani pekee.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Jones Olotu, amesema mradi huo ni sehemu ya utekelezaji wa mpango wa nishati (Energy Compact) unaolenga kufikisha umeme kwa wananchi wote ifikapo 2030, ikiwa ni pamoja na kuunganisha wateja wapya takriban milioni 8.
Kwa Mkoa wa Mwanza, visiwa 65 vitanufaika kwa gharama ya Shilingi bilioni 4.8, ambapo Serikali tayari imetoa Shilingi bilioni 3.3 na kiasi kilichobaki kitalipwa na wananchi kwa utaratibu wa ruzuku.
Mikoa itakayonufaika ni Mwanza, Geita, Kagera, Mara, Rukwa, Lindi, Mtwara na Pwani.


