Na mwandishi wetu, Gazetini
MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) imesifu matumizi sahihi ya fedha za kodi za Watanzania katika Mradi wa Bwawa la Julius Nyerere kufuatia ziara yake ya kikazi ya Februari 14, 2026, ikieleza kuwa mradi huo unaonyesha namna kodi zinavyochochea maendeleo kwa kuongeza upatikanaji wa umeme wa uhakika nchini.
Ziara hiyo ilihusisha viongozi na maafisa wa Elimu na Mawasiliano kutoka vituo vyote vya mamlaka hiyo nchini, wakiwa na lengo la kujifunza na kujionea namna kodi za wananchi zilivyowezesha utekelezaji wa mradi huo mkubwa wa kimkakati wa taifa.
Akizungumza mara baada ya ziara hiyo, Mkurugenzi wa Elimu na Mawasiliano wa TRA, Richard Kayombo, amesema ziara katika Mradi wa Bwawa la Julius Nyerere ilikuwa muhimu kwa kuwa TRA ndiyo taasisi inayokusanya kodi, hivyo walitaka kujionea jinsi fedha za wananchi zinavyotumika na matokeo yake kwa maendeleo ya nchi.
Bw. Kayombo alisema mradi huo unaonyesha jinsi kodi zinavyobadilisha maisha ya wananchi kwa kuongeza umeme wa uhakika, kukuza biashara, uwekezaji na ukuaji wa uchumi, hivyo kupanua wigo wa ukusanyaji wa mapato ya Serikali.
Aliongeza kuwa ongezeko la uzalishaji wa umeme nchini linasaidia kupunguza changamoto za mgao wa umeme na kuimarisha utoaji wa huduma kwa wananchi na sekta binafsi.
“Mradi huu unatupa ushahidi kuwa kodi za wananchi zinapotumika ipasavyo huleta matokeo makubwa yanayoonekana na kugusa maisha ya jamii moja kwa moja,” amesema Kayombo.
Kwa upande wao, maafisa wa Elimu na Mawasiliano wa TRA walisema ziara hiyo imewapa uelewa mpana kuhusu uwekezaji uliofanywa na Serikali katika sekta ya nishati na kuahidi kuwa mabalozi wazuri wa kuhamasisha ulipaji wa kodi kwa hiari na kwa wakati.
Aidha, wameahidi kuendelea kuwaelimisha wananchi kuwa kodi wanazolipa zina mchango mkubwa katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo, mfano Bwawa la Julius Nyerere, ambalo sasa ni moja ya vyanzo muhimu vya umeme katika Gridi ya Taifa, likichangia takribani megawati 2,115.
Akizungumza kwa niaba ya uongozi wa kituo, Kaimu Meneja Uendeshaji na Udhibiti wa Mifumo wa Kituo cha Kuzalisha Umeme cha Julius Nyerere, Elinainyi Kalalu, alisema ziara hiyo imekuwa na tija kwa kuwa imewapa fursa ya kujionea namna fedha za wananchi zinavyotumika na matokeo yake kurejea kwa wananchi kupitia huduma bora ya umeme.
“Ziara hii imekuwa na tija kubwa. Napenda kusisitiza kuwa kituo kitaendelea kuzalisha umeme kwa weledi na ufanisi ili kuhakikisha huduma ya uhakika kwa wananchi. Ni muhimu pia kwa TRA kuendelea kuhamasisha ulipaji wa kodi, kwani ndizo zinazoziwezesha Serikali kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo nchini,” alisisitiza Kalalu.
Ziara hiyo imekuwa ya mafanikio kwani imeimarisha uelewa kwamba ulipaji wa kodi kwa hiari na kwa wakati ni msingi wa utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo, ikiwemo uwekezaji katika sekta muhimu ya nishati ya umeme kwa ustawi wa Taifa.


