Na mwandishi wetu, Gazetini
WAZIRI wa Nishati, Deogratius Ndejembi, amesema wilaya za Urambo na Kaliua mkoani Tabora zipo tayari kupokea uwekezaji, hususan wa viwanda, kutokana na upatikanaji wa umeme wa uhakika unaotosheleza mahitaji ya sasa na ya baadaye.
Ndejembi ametoa kauli hiyo Februari 14, 2026 wakati akikagua mradi wa njia ya kusafirisha umeme wa msongo wa kilovoti 132 kutoka Tabora hadi Urambo pamoja na Kituo cha Kupoza na Kusambaza Umeme cha Uhuru – Urambo chenye uwezo wa megawati 24.
Alisema uwezo wa kituo hicho unazidi mahitaji ya sasa, ambapo matumizi ya umeme katika wilaya za Urambo na Kaliua ni megawati 2.5 mchana na huongezeka hadi megawati 7 usiku, hali inayoonesha uwepo wa fursa kubwa kwa wawekezaji.
“Urambo ipo tayari kwa uwekezaji. Umeme uliopo unatosha na hata kuzidi mahitaji ya sasa, hivyo ni fursa kwa wawekezaji kuanzisha viwanda na shughuli nyingine za kiuchumi,” amesema Ndejembi.
Aliongeza kuwa Serikali chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imejipanga kuhakikisha kunakuwa na umeme wa uhakika nchini ili kuchochea ukuaji wa uchumi na uwekezaji, hususan katika maeneo ya kilimo kama Urambo na Kaliua, ambayo yanazalisha zao la tumbaku linalohitaji viwanda vya kuongeza thamani.
Aidha, amesema Serikali imetoa zaidi ya Sh trilioni 1.9 kupitia Tanesco kwa ajili ya Mradi wa Gridi Imara, unaolenga kuimarisha usambazaji wa umeme nchini.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, Lazaro Twange, alisema mradi huo wa Sh bilioni 44 ulianza Septemba 2021 na kukamilika kwa asilimia 100, huku kituo kikianza kufanya kazi Machi 2025, hatua inayotarajiwa kuchochea maendeleo ya viwanda na uwekezaji katika ukanda huo.


