LOS ANGELES, Marekani
BIBIYE mwenye jina kubwa katika muziki wa R&B nchini Marekani, Beyonce, ambaye pia ni mke wa rapa Jay Z, amekutwa na kitu kizito baada ya kupoteza wafuasi (followers) milioni 10 katika akaunti yake ya mtandao wa kijamii wa Instagram.
Mashabiki wameamua kujiondoa kwenye akaunti yake baada ya mumewe, Jay Z, kuhusishwa na mfanyabiashara mwenye kashfa za unyanyasaji wa kingono, Epstein.
Tangu Epstein alipofariki mwaka 2019 akiwa gerezani kusubiri hukumu, zimekuwa zikiibuka taarifa zinazowataja watu maarufu kuwa na ukaribu naye, wakihisiwa kuwa huenda nao walishiriki unyanyasaji wa kingono.
Miongoni mwa walioibuliwa ni Rais wa Marekani, Donald Trump, ambaye hata hivyo amekana kuhusika katika uhalifu wa Epstein, licha ya kukiri aliwahi kuwa rafiki yake wa karibu.
Kwa upande mwingine, pia orodha ndefu hiyo ya ‘marafiki’ wa Epstein haijaliacha jina la aliyewahi kuwa Rais wa Marekani, Bill Clinton.
Hivi karibuni, Beyonce aliandika historia ya kuingia katika orodha ya wanamuziki watano pekee duniani wenye hadhi ya kuitwa mabilionea.
Akiwa na umri wa miaka 44 kwa sasa, Beyonce anaungana na Jay Z, ambaye alishatangulia kuingia kwenye listi hiyo miaka michache iliyopita.


