NEW DELHI, India
UHABA wa wafanyakazi unaoikumba Urusi kwa sasa umegeuka fursa kwa raia wa India, ambao sasa wanamimilika kwa wingi nchini humo.Raia wa India takribani 40,000 wanataarajiwa kuingia Urusi mwaka huu. Wengine kati ya 70,000 hadi 80,000 walikuwa wameshaingia Urusi kufikia mwishoni mwa mwaka 2025.
Mwitikio huo ni zao la Mkutano uliowakutanisha Waziri Mkuu wa India, Narendra Modi, na Rais wa Urusi, Vladimir Putin.
Katika mkataba waliosaini, walikubaliana kuwa India ingepeleka wafanyakazi zaidi ya 70,000 nchini Urusi kufikia mwishoni mwa mwaka huu.
Kivutio kikubwa kwa raia wa India wanaoingia Urusi ni mishahara minono wanayolipwa, ambayo ni kati ya Dola 555 hadi Dola 1,111 kwa mwezi.
Mwishoni mwa mwaka 2025, Gazeti la Fontanka la Urusi liliripoti juu ya raia wa India waliokuwa wakifanya kazi ya kufagia barabara mjini St. Petersburg.
Kwa mujibu wa kile kinachoelezwa na Gazeti hilo, mshahara wao ni Dola 1,316 kwa mwezi, achilia mbali kugharamiwa chakula, fedha za kujikimu na masomo ya kujifunza lugha ya Kirusi.
Hata hivyo, wakosoaji wanahusisha mpango wa ajira za Urusi kwa raia wa India na mgogoro unaoendelea kati ya Taifa hilo na Ukraine.
Kwamba baadhi ya raia wa India huishia kupelekwa katika vita huko Ukraine, madai ambayo hata hivyo yameendelea kukanushwa na mamlaka za Urusi.
Taarifa zinadai kuwa raia wa India 126 walipelekwa kuwasaidia wanajeshi wa Urusi nchini Ukraine, ambapo 12 walipoteza maisha na wengine 96 walirudi nyumbani.


