Na mwandishi wetu, Gazetini
WASANII wa muziki wa Nigeria wamezibeba kwa wingi tuzo za Afrima, ambazo hafla yake ilifanyika Januari 11, 2026.
Wakati huo huo, usiku wa tuzo hizo haukumalizika bila kutajwa kwa Bongo Fleva, ambapo staa wa muziki huo, Juma Jux, alitwaa tuzo ya Msanii Bora wa Afrika Mashariki.
Kwa Nigeria, mkali wa Afrobeat, Burna Boy, aliibeba tuzo ya Albamu Bora ya Mwaka kupitia ‘No Sign of Weakness’.
Pia, mkali huyo aliibeba ile ya Kolabo Bora ya Mwaka, akigawana na Shallipopi, ambaye pia alitwaa tuzo ya Wimbo Bora kupitia ‘Laho’.
Hata hivyo, kiboko yao usiku huo ni Rema, ambaye alinyakua tuzo tatu; Msanii Bora wa Mwaka, Msanii Bora wa Kiume wa Afrika ya Magharibi, na Msanii Bora wa RnB na Soul.
Nigeria haikuishia hapo. Staa Yemi Alade alitangaza kuwa mshindi wa kipengele cha Wimbo Bora uliotumika kwenye muvi, ambao ni ‘You Are’ uliotumika katika tamthilia ya ‘Iyanu’.
Kama hiyo haitoshi, Phyno alitwaa tuzo ya Msanii Bora wa Hip Hop ya Afrika, wakati ile ya Chipukizi Bora ikienda kwa Oing Madi, na Chella akitangazwa kuwa mshindi wa tuzo ya Chaguo la Mashabiki.
Nje ya Nigeria, mwanamuziki wa Ghana, Wendy Shay, ndiye aliyeibeba tuzo ya Msanii Bora wa Kike kwa upande wa Afrika ya Magharibi.
Pia, mkali wa Afrika Kusini, Nontokozo Mkhize, alijiondokea na tuzo ya Msanii Bora wa Kike kwa upande wa Kusini kwa Afrika.


