13.9 C
New York

Dhambi ya usaliti inamtafuna Nicolas Sarkozy?

Published:

Na mwandishi wetu, Gazetini
HIVI karibuni, Mahakama ya Uhalifu ya Paris, Ufaransa, ilimuhukumu kifungo cha miaka mitano gerezani aliyewahi kuwa Rais wa nchi hiyo, Nicolas Sarkozy.
Hukumu hiyo imekuja baada ya Sarkozy kukutwa na hatia katika mashitaka ya kujinufaisha na fedha kutoka kwa aliyekuwa Rais wa Libya, Kanali Muammar Gaddafi.
Sarkozy ametajwa kufanya hivyo kati ya mwaka 2005 na 2007, ikielezwa kuwa alizitumia fedha hizo kuendesha kampeni zake za kuwania kiti cha urais.
Kwa hukumu hiyo, Sarkozy mwenye umri wa miaka 70, anaandika historia ya kuwa rais mstaafu wa kwanza kupelekwa jela katika historia ya siasa za Ufaransa.
Sarkozy ni nani?
Ni Rais wa zamani wa Ufaransa, ambaye aliliongoza Taifa hilo kuanzia mwaka 2007 hadi 2012. Kabla ya urais, alikuwa kiongozi wa Chama cha Union for a Popular Movement (UMP), pia akiwahi kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani chini ya Rais Jacques Chirac.
Mwaka 2017, Sarkozy aliachana na siasa, ingawa huo ukawa mwanzo wa maisha magumu ya kuandamwa na mashitaka mbalimbali, yakiwamo ya kujihusisha na rushwa.
Mashitaka yaliyompeleka gerezani
Januari, mwaka huu, waendesha mashitaka nchini Ufaransa waliibua madai ya Sarkozy kuingia makubaliano yasiyo halali na Gaddafi.
Kwamba Sarkozy alipewa kiasi cha fedha kwa ajili ya kampeni zake za urais, huku akiwa na jukumu la kuiunga mkono Serikali ya Gaddafi iliyokuwa ikipingwa na jumuhiya za kimataifa.
Mbali ya Sarkozy, mashitaka hayo yaliwahusu pia watu wengine 11, akiwamo aliyekuwa meneja wa masuala ya fedha wakati wa kampeni, Eric Woerth.
Ushahidi umetoka Libya
Mwaka 2011, moja ya mashirika ya habari nchini Libya liliripoti kuwa Serikali ya Gaddafi ilimpa Sarkozy kiasi kikubwa cha fedha kwa ajili ya kampeni zake za urais katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2007.
Mwaka 2012, Gazeti la mtandaoni la Ufaransa, Mediapart, lilifichua nyaraka za siri zilizoonesha makubaliano ya Gaddafi kumpatia Sarkozy kiasi cha Dola za Marekani milioni 52 kwa ajili ya kuwezesha kampeni zake za urais nchini Ufaransa.
Mwaka 2014, kituo cha televisheni cha Ufaransa, France 24, kiliibua nukuu ya Gaddafi (kabla ya kifo chake) akisema: “Sarkozy anapaswa kunishukuru. Tulimpa fedha zilizompa ushindi.”
Mwaka huo huo, mtoto wa Gaddafi, Saif al-Islam Gaddafi, aliibua hoja ya aina hiyo akisema wanamuomba Sarkozy kurejesha fedha za Walibya (alizopewa na Gaddafi).
Mwaka 2016, mfanyabiashara wa Ufaransa mwenye asili ya Lebanon, Ziad Takieddine (sasa marehemu), alikiri kusimamia malipo ya Dola milioni 2.5 kutoka Libya kwenda kwa Sarkozy.
Dhambi ya usaliti?
Iko wazi na hakuna ubishi kuwa wakati fulani Sarkozy na Gaddafi waliwahi kuwa marafiki wazuri katika ulimwengu wa siasa za kimataifa.
Ikumbukwe, mwaka 2007, baada ya kuingia madarakani, Sarkozy hakuchelewa akumualika Gaddafi katika Ikulu ya Ufaransa jijini Paris.
Hata hivyo, wakati wa vuguvugu la kumng’oa madarakani Gaddafi mwaka 2011, Sarkozy alimgeuka na kuyaunga mkono mataifa ya Ulaya yaliyoivamia Libya.
Je, kinachomkuta Sarkozy kwa sasa ni matokeo ya dhambi ya usaliti aliomfanyia rafiki yake huyo? Ndiyo, Sarkozy anaamini watu wa karibu wa Gaddafi wamelipiza kisasi.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img