RABAT, Morocco
MSIMU huu wa fainali za Mataifa ya Afrika kwa soka la Wanawake utafikia ukomo Jumapili hii, yaani Agosti 16, 2026. Michuano hiyo inafanyika Morocco.
Safari hii, ni timu ya soka ya Taifa ya Wanawake ya Cameroon dhidi ya wenzao wa Malawi. Timu zote zinasaka taji hilo kwa mara ya kwanza.
Cameroon walitinga hatua hii ya mwisho baada ya ushindi wa penalti dhidi ya wenyeji Morocco, mchezo uliofika hadi dakika 120. Malawi wao waliitoa Algeria kwa kichapo cha mabao 3-1.
Malawi wanaoshiriki michuano hiyo kwa mara ya kwanza, walionesha maajabu walipopata ushindi wa 3-2 dhidi ya mabingwa mara 10, Nigeria.
Wakiwa Kundi C, pia waliifunga Misri mabao 3-1, kisha kufungwa 2-1 na Zambia. Walimaliza wakiwa kileleni mwa Kundi.
Katika hatua ya robo fainali, walikutana na Ghana na kuitandika mabao 2-1, kabla ya ushindi wa 3-1 katika nusu fainali yao dhidi ya Algeria.
Kwa upande wao, Cameroon walianza mashindano wakiwa Kundi D. Walizifunga Mali (2-1), Ghana (1-0), kabla ya sare (1-1) walipokutana na Cape Verde.
Walipoingia robo fainali, waliifunga Nigeria bao 1-0, kabla ya ushindi wa penalti 3-1 dhidi ya Morocco, mchezo ambao dakika 120 zilimalizika kwa timu hizo kutokufungana.
Kuelekea fainali, Cameroon inapaswa kuwachunga ndugu wawili, Tabitha na Temwa Chawinga, ambao ndiyo wachezaji tegemeo katika kikosi cha Malawi.
Kila mmoja aliingia kambani (Tabitha akifunga mawili) katika ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Algeria. Temwa ndiye kinara wa mabao msimu huu, akiwa amezifumania nyavu mara tano na asisti mbili.
Hata hivyo, washambuliaji hao wanafahamu kuwa haitakuwa rahisi safari hii. Cameroon inajivunia ubora wa kipa wake mwenye umri wa miaka 22, Michaely Bihina.
Katika mchezo dhidi ya Nigeria, licha ya Cameroon kushinda bao 1-0, Bihina alifanya kazi ya ziada langoni, akiokoa mabao tisa ya wazi.
Kama hiyo haitoshi, kipa huyo aliyejiunga na Benfica mwanzoni mwa mwaka 2026 aliokoa penalti nne katika nusu fainali yao dhidi ya Morocco.


