28.2 C
New York

Prof. Kabudi aongoza ibada ya kumaliza msiba wa Lukuvi

Published:

WAZIRIi wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), Prof. Palamagamba Kabudi, ameongoza viongozi mbalimbali katika Ibada ya Misa Takatifu ya kumaliza msiba wa aliyewahi kuwa Waziri wa Nchi katika Ofisi hiyo, Marehemu William Vangimembe Lukuvi.

Ibada hiyo imefanyika leo, Agosti 15, 2026, katika Kijiji cha Idodi, Kata ya Idodi, mkoani Iringa, ikihudhuriwa na viongozi mbalimbali, ndugu, jamaa na wananchi waliofika kutoa heshima na kuungana na familia katika kipindi cha maombolezo.

Marehemu William Lukuvi alizaliwa Agosti 15, 1955, katika Kijiji cha Mapogoro, Kata ya Idodi, Wilaya ya Iringa Vijijini. Alianza elimu ya msingi katika Shule ya Msingi Kitanewa kabla ya kujiunga na Chuo cha Ualimu Tabora na kupata Cheti cha Ualimu. Baadaye alisoma Sayansi ya Siasa nchini Urusi, akapata Shahada ya Masuala ya Kimataifa na Diplomasia na baadaye Shahada ya Uzamili ya Sayansi ya Siasa kutoka Chuo Kikuu Huria cha Tanzania. (Prime Minister’s Office Tanzania)

Lukuvi alianza safari yake ya kisiasa mwaka 1973 alipojiunga na TANU akiwa mwanafunzi, na baadaye akashika nafasi mbalimbali ndani ya CCM, ikiwamo Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana wa CCM. Pia aliwahi kuwa Mkuu wa Wilaya ya Bukoba na Mkuu wa Mikoa ya Dodoma na Dar es Salaam.

Mwaka 1995 alichaguliwa kuwa Mbunge wa Jimbo la Isimani, nafasi aliyoitumikia kwa takribani miaka 30 hadi alipofariki. Katika Serikali, aliwahi kuwa Naibu Waziri wa Vijana na Ajira, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi. Mwaka 2023 aliteuliwa kuwa Mshauri wa Rais katika masuala ya Siasa na Uhusiano wa Jamii.

Katika utumishi wake, Lukuvi alikumbukwa kwa kusimamia masuala mbalimbali ya maendeleo, ikiwamo utoaji wa hati za ardhi, mifumo ya kidijitali katika huduma za ardhi na mipango ya matumizi ya ardhi. Pia akiwa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, alisimamia hatua mbalimbali za upanuzi wa mji na ujenzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM). (Prime Minister’s Office Tanzania)

Lukuvi alifariki dunia Machi 25, 2026, akiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Benjamin Mkapa mkoani Dodoma, akiwa na umri wa miaka 70. (Prime Minister’s Office Tanzania).

Related articles

Recent articles