21.8 C
New York

Waziri Kabudi: Serikali itaendelea kuthamini mchango wa Lukuvi

Published:

Na mwandishi wetu, Gazetini

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi, amesema Serikali itaendelea kuheshimu na kuthamini mchango wa kiuongozi uliotolewa na aliyekuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), Marehemu William Lukuvi.

Hayo ameyasema Agosti 15, 2026, wakati wa maadhimisho ya ibada ya Misa Takatifu ya kumaliza msiba iliyofanyika nyumbani kwa marehemu, Idodi, mkoani Iringa, na kuhudhuriwa na wananchi pamoja na viongozi mbalimbali wa chama na Serikali.

“Enzi za uhai wake, Waziri Lukuvi alinisaidia kufahamu shughuli mbalimbali za Bunge na Serikali na hivyo kupata weledi mzuri katika mambo mengi kutokana na uzoefu aliokuwa nao,” amesema.

Aidha, uwezo wake wa kusimamia nidhamu ipasavyo Bungeni, ikiwa ni pamoja na kuimarisha mahusiano kati ya Serikali na Bunge, ulimfanya aendelee kuaminiwa katika nafasi ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu.

Kwa upande wake, Mama Germana Lukuvi, mjane wa marehemu, ameishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kushikamana na familia tangu walipopata msiba.

Awali, Mbunge wa Isimani, Emanuela Mtatifikolo, amesema Marehemu Lukuvi ataendelea kuishi katika mioyo ya wananchi wa Isimani kutokana na mageuzi makubwa ya maendeleo aliyoyafanya.

“Uwakilishi wake kwa wananchi wa Jimbo la Isimani na kwa kushirikiana na Serikali, aliwezesha Jimbo la Isimani kunufaika na ujenzi wa barabara za lami, uimarishaji wa huduma za afya na kuendelea kuboresha miundombinu ya elimu sambamba na umeme,” amebainisha.

Related articles

Recent articles