6.4 C
New York

Bandari ya Dar es Salaam yaanza kuhudumia meli kubwa zaidi

Published:

Na Mwandishi Wetu, Gazetini

MALENGO ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) ya kuifanya Bandari ya Dar es Salaam kuwa kitovu (hub) cha kuhudumia shehena ya mizigo ya kimataifa yanayoelekea nchi jirani yameanza kuzaa matunda, baada ya bandari hiyo kuanza kupokea na kuhudumia meli kubwa zenye urefu wa hadi mita 300.

Hatua hii imefanikishwa na maboresho makubwa ya miundombinu yaliyotekelezwa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kupitia mradi wa maboresho wa Dar es Salaam Maritime Gateway Project (DMGP).

Kwa mara ya kwanza katika historia yake, Bandari ya Dar es Salaam imehudumia meli kubwa aina ya Post Panamax, MV. MYNY, yenye urefu wa mita 300, uzito wa tani 75,201 na uwezo wa kubeba makasha 6,840.

Mkurugenzi wa Marini na Shughuli za Kibandari, Kapteni Abdallah Mwingamno, akizungumza leo Ijumaa Septemba 5, 2025 amesema ujio wa meli hiyo unathibitisha uwezo mpya wa bandari hiyo kuhudumia meli kubwa na za kisasa.
“Mafanikio haya ni matokeo ya maboresho makubwa ya miundombinu na uwekezaji wa mitambo ya kisasa kupitia TPA. Hii ni ishara kwamba bandari yetu sasa imejiweka kwenye ramani ya ushindani wa kikanda na kimataifa,” amesema.

Kupitia DMGP, Serikali imeboresha gati namba 1–7 kwa kuongeza kina kutoka mita 8 hadi 14.5, sambamba na kuimarisha eneo la kugeuzia meli kwa kina cha mita 15, huku lango la kuingilia likipanuliwa. Pia, gati maalumu la kuhudumia meli za magari (RoRo Berth) limejengwa, mtandao wa reli umeimarishwa na mfumo wa umeme kusimikwa.

Mradi huo wenye thamani ya Sh trilioni 1.118 unafadhiliwa na Benki ya Dunia, wafadhili pamoja na mapato ya ndani ya TPA.

Kwa maboresho haya, Bandari ya Dar es Salaam sasa imepiga hatua kubwa kuelekea kuwa kitovu cha usafirishaji na biashara katika Afrika Mashariki na Kati, ikichochea maendeleo ya kiuchumi ya Tanzania na ukanda mzima.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img