27.5 C
New York

Porro: Kufuzu fainali ni ndoto iliyotimia

Published:

NEW YORK, Marekani

BEKI wa Hispania na mchezaji bora wa mechi, Pedro Porro, amesema kufuzu kwa timu yake fainali ni ndoto aliyokuwa akiisubiri kwa muda mrefu, akieleza kuwa ushindi dhidi ya Ufaransa umetokana na mshikamano wa kikosi kizima.

Akizungumza baada ya mchezo, Porro alisema Hispania ilicheza kwa nidhamu na kutekeleza mpango wake tangu mwanzo hadi mwisho.

“Hii ni ndoto iliyotimia kwangu. Ilikuwa ndoto yangu kubwa zaidi. Nina furaha sana kwa timu. Tulicheza vizuri kuanzia mwanzo hadi mwisho na leo tulifanya kila tulichoweza ili kufuzu,” alisema.

Amesema walikuwa wakifahamu wanakutana na mpinzani mwenye uwezo mkubwa, lakini walifanikiwa kutekeleza mkakati waliouandaa.

“Tulijua tunakutana na timu ngumu sana. Huu ni ushindi wa timu nzima, si wangu pekee. Nawapongeza wachezaji wote kwa kiwango walichoonyesha,” amesema.

Porro alieleza kuwa kumiliki mpira kulikuwa sehemu muhimu ya mbinu zao za kuwadhibiti Wafaransa, ambao nguvu yao kubwa ni mashambulizi ya kushtukiza.

“Tulijua kumiliki mpira kungetusogeza karibu na ushindi. Mashambulizi yao ya kushtukiza ndiyo silaha yao kubwa, na kuyazuia ilikuwa jambo muhimu,” amesema.

Kuhusu kutolewa kwake uwanjani, Porro amesema alihisi hangeweza kuendelea kutoa mchango mkubwa kutokana na uchovu, akisisitiza kuwa mafanikio hayo ni ya kikosi kizima.

“Nilihisi siwezi kuchangia zaidi. Ushindi huu umeletwa na wachezaji wote 26. Sasa tunaelekeza nguvu zetu kwenye fainali,” amesema.

Ameongeza kuwa licha ya uchovu baada ya mechi ngumu, Hispania itajipanga upya na kupambana kwa nguvu zote katika mchezo wa fainali.

Related articles

Recent articles