30.8 C
New York

Mtanzania anyakua tuzo ya uandishi bora wa filamu ya malaria Marekani

Published:

Na mwandishi wetu, Gazetini

MTANZANIA, Gloria Majule, ameendelea kuiwakilisha vyema Tanzania katika jukwaa la kimataifa la sanaa baada ya kuibuka mshindi wa tuzo ya uandishi bora wa filamu inayohusu ugonjwa wa malaria nchini Marekani.

Gloria, ambaye ni mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Cornell nchini Marekani na mwenye shahada mbili, alitwaa tuzo hiyo kwa msimu wa mwaka 2025/2026 baada ya kushindana na washiriki zaidi ya 1,000 kutoka mataifa mbalimbali duniani.

Mafanikio hayo yamempa nafasi ya kutembea kwenye zulia jekundu (Red Carpet) katika hafla maalum ya utoaji wa tuzo hiyo, huku ushindi wake ukiendelea kutajwa kama hatua kubwa kwa sanaa ya Tanzania katika jukwaa la kimataifa.

Gloria, ambaye ni mtoto wa Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Dodoma, Dk. Neema Majule, ameandika jina lake katika historia ya tuzo hiyo kwa kuwa miongoni mwa Waafrika wachache kufikia mafanikio hayo, akitajwa kuwa Mwafrika wa pili kushinda tuzo hiyo ya kimataifa ya uandishi wa filamu.

Filamu hiyo aliyoandika inaangazia changamoto ya ugonjwa wa malaria, ambao bado ni tishio kubwa kwa afya ya jamii hasa katika nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara, ikiwemo Tanzania.

Kupitia kazi hiyo ya sanaa, Gloria ameweza kuwasilisha ujumbe wa kijamii unaolenga kuongeza uelewa kuhusu athari za malaria, umuhimu wa kinga na jitihada za kukabiliana na ugonjwa huo unaoendelea kuathiri mamilioni ya watu duniani.

Baada ya ushindi huo, filamu hiyo imeendelea kupata umaarufu nchini Marekani, huku mabango yanayotangaza kazi hiyo na mafanikio ya Gloria yakiwa yamewekwa katika maeneo mbalimbali jijini New York.

Mafanikio ya Gloria yanaongeza sura mpya ya uwezo wa wasanii na wabunifu Watanzania katika kutumia sanaa kama chombo cha kuelimisha jamii, kuibua changamoto za kijamii na kuipeleka Tanzania katika ramani ya kimataifa.

Related articles

Recent articles