23.1 C
New York

Vigogo walioangukia pua Kombe la Dunia 2026

Published:

BOSTON, Marekani

NI timu nne pekee zilizobaki katika fainali za Kombe la Dunia za mwaka huu (2026). Kwamba timu 44 zimeshaaga mashindano hayo ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA).

Wakati timu kama Cape Verde, Jordan na Uzbekistan zikifurahia kushiriki tu, zipo zilizokuwa na matumaini ya kufanya vizuri lakini ziliangukia pua.

UJERUMANI

Mabingwa wa Kombe la Dunia mwaka 2014. Hawajashinda mechi ya hatua ya mtoano tangu kipindi hicho na safari hii walitolewa na Paraguay.

Kutokana na mambo yalivyokwenda, wamemtimua kocha na nafasi yake kuchukuliwa na Jurgen Klopp aliyewahi kuinoa Liverpool.

BRAZIL

Safari yao iliishia hatua ya 16 Bora, ambapo waliondoshwa na Norway ya Erling Haaland. Kukosekana kwa Rodrigo na Eder Militao walioumia kabla ya mashindano kuliiharibia Brazil.

Chini ya kocha Carlo Ancelotti mwenye mkataba hadi mwaka 2030, kikosi hicho kinatarajiwa kuwa na mabadiliko makubwa, hasa baada ya Neymar kustaafu na umri kuwatupa mkono Marquinhos, Casemiro na Alisson.

MAREKANI

Wenyeji hao chini ya kocha raia wa Argentina, Mauricio Pochattino, walitarajiwa kufika mbali, walau hatua ya robo fainali.

Hata hivyo, safari yao ilikwamia hatua ya 16 Bora baada ya kupoteza mchezo wao dhidi ya Ubelgiji.

KOREA YA KUSINI

Katika kundi lililokuwa na Afrika Kusini, Czech na Mexico, Korea ya Kusini ilikuwa na nafasi kubwa ya kuvuka na kuingia hatua ya 16 Bora.

Kinyume cha matarajio hayo ya wengi, timu hiyo iliishia makundi. Waliifunga Czech, kisha ikafungwa mechi mbili mfululizo.

AFRIKA

Timu nane kati ya 10 za Afrika zilivuka makundi na kuingia hatua ya 32 Bora. Hata hivyo, ni Misri na Morocco tu zilizotinga 16 Bora.

Hata hivyo, Misri ilishindwa kwenda robo fainali baada ya kufungwa na Argentina, wakati Morocco iling’olewa na vigogo Hispania.

URUGUAY

Katika kundi lililokuwa na Saudi Arabia na Cape Verde, wengi walitarajia kuona Uruguay ikiungana na Hispania katika nafasi mbili za kuingia hatua ya 16 Bora.

Hata hivyo, Uruguay walishangaza wengi kwa kuishia kwao makundi, ikifanya hivyo kwa mara ya pili mfululizo baada ya mwaka 2022.

Related articles

Recent articles